ZECO: Waliojenga chini ya umeme mzito hawataungiwa
Na Mwanajuma Abdi
3 OCTOBER 2010 JUMAPIL.I
SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO), limesema halitowapatia huduma wananchi wataojenga katika maeneo yaliyopita njia kuu ya umeme licha ya kuwa na vibali halali vya ujenzi wa nyumba zao.
Hayo yamesemwa jana na Mwanasheria wa ZECO, Ali Hamad wakati akitoa ufafanuzi katika masuala mbali mbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari katika semina ya siku moja, iliyoandaliwa na Shirika hilo kwa vyombo vya habari huko katika ukumbi wa Eacrotanal mjini Unguja.
Alisema kuna baadhi ya wananchi wanaojenga chini ya waya zenye umeme mzito wa 32KV (32,000 voti) na 11KV (11,000 voti) ambao wamewaonyesha vibali halisi vya ujenzi kutoka mamlaka husika.
Alieleza ZECO itaendelea na kuwanyima huduma hiyo licha ya kukosa fedha, lakini pia wanazingatia usalama wa wananchi waliojenga katika eneo hilo.
Aidha alifafanua kuwa, kwa wale wateja waliobahatika kuungiwa umeme katika maneo yaliyopita waya mkubwa watendelea kuwa nayo lakini pia wataendelea kupata madhara ya kiafya.
Alifahamisha kuwa, tayari wameshafanya vikao vya pamoja na mamlaka zinazohusika na utoaji wa viwanja, lakini bado tatizo hilo linaendelea.
Kaimu Mkaaguzi Mkuu wa Ufundi, Khalfan Salum alisema waya huo mkubwa unaathari kubwa kwa binaadamu kwani ndani yake inatoka miozi, ambayo inapenda hadi navu za ubongo.
Alisema kwamba, waya wa umeme 33KV nyumba inatakiwa ijengwe kwa masafa ya mita 50 na 11KV inatakiwa ujenzi wa makaazi yajengwe kwa mita 15 ili kujiepusha na athari ya miozi na madhara mengine ikiwemo vifo vya kuangukiwa na nguzo.
Nae, Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme, Hassan Ali Mbarouk alisema ZECO, limeandaa mkakati wa kuwapatia huduma ya umeme wateja wapya kwa mwezi mmoja badala ya kukaa kwa muda mrefu kusubiri huduma hiyo.
Alieleza huduma hiyo wakipatiwa wateja hao watawekewa mita za TUKUZA, ambazo zimeonekana wateja wanazifurahia zaidi kuliko mita za kawaida katika kuzitumia.
Mbarouk alisema mikakati mengine ni kuzifanyia tathmini na kuzipima transfoma 500 za Unguja ili kujua uwezo wake kuwahudumia wateja, sambamba na kuondoa umeme mdogo katika baadhi ya maeneo.
Shirika la Umeme Zanzibar linawaateja 87,000 Zanzibar, ambapo kati ya hao wateja 73,000 wapo Unguja na kati ya hao 26,000 wanatumia mita za TUKUZA na Pemba mita hizo zimefikia 5,000 kwa sasa na 9,000 ni mita za kawaida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment