TAMWA yalaani udhalilishwaji wagombea wanawake
Na Muandishi Wetu
2 october 2010
WAGOMBEA wanaume ambao wanatoa lugha za matusi kwa wagombea wanawake majimboni, wanadhihirisha kutokuwa na hoja wala sera za maendeleo na hivyo wanastahiki kunyimwa kura.
Hivi karibuni baadhi ya wanaume ambao wanaona wagombea wanawake ni tishio kwao, wamekuwa wakiwaundia mbinu chafu ikiwa ni pamoja na kuwakejeli na kuwadhalilisha kwa matusi.
Wanawake kadhaa wanaogombea Ubunge majimboni wamelalamika kuwa baadhi ya wanaume wapinzani wao wamekuwa wakiwatukana na kuwakejeli baada ya kubaini kuwa wagombea hao wanawakake wanakubalika zaidi yao.
Miongoni mwa majimbo ambayo wagombea wanaume wamelalamikiwa kutumia lugha za matusi dhidi ya wagombea wanawake ni pamoja na jimbo la Kawe, Dar es Salaam na Kwimba mkoani Mwanza.
Sheria ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002, kifungu cha 89 kifungu kidogo cha kwanza (a) kinasema kuwa mtu yeyote akitoa lugha ya matusi kwa mtu mwingine ni kosa na adhabu yake ni miezi sita jela.
Kutokana na hali hiyo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimewaonya wanaogombea uongozi mwaka huu kupitia vyama vyote vya siasa, na kueleza kuwa Watanzania wameelimika na zama za kuwanyanyasa wanawake na kuwanyima haki ya kuwa viongozi zimepitwa na wakati.
Katika taarifa ya Chama hicho iliyoasaini na Mkurugenzi Mtendaji Ananilea Nkya, ilieleza kuwa wagombea wanaume ambao bado wana mitazamo potofu dhidi ya wanawake, wajitoe kwenye uchaguzi kwani Watanzania wamechoka kuvumilia udhalilishwaji wa wanawake.
Nkya alisema Watanzania wanachohitaji ni mtu mwenye sifa za uongozi awe mwanamke au mwanaume bila kujali ameoa au kuolewa kutokana kuwepo watu wengi waliooa na kuolewa lakini hawana uadilifu katika ndoa zao.
Jumla ya wanawake 190 wanagombea Ubunge Majimboni mwaka huu wakiwepo 25 CHADEMA, 24 CCM, 15 NCCR Mageuzi, CUF 14 , UDP 14, UPDP 14, TADEA 12, DP 11 na UMD 10. Waliobaki wanagombea kupitia vyama vya NLD, NRA, SAU, TLP, Jahazi Asilia, Makini, Chausta, APPT-Maendeleo na AFP. Kadhalika wanawake 557 wanagombea udiwani majimboni.
Monday, 4 October 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment