Washauri mapitio sheria wanaotesa wanyama
Na Halima Abdalla
4 OCTOBER 2010
SERIKALI imeshauriwa kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na utesaji wanyama kwa nia ya kuwabana watu wanaowatesa wanyama ili iwe fundisho kwa wanaotenda vitendo hivyo.
Ushauri huo umetolewa na Katibu wa Jumuiya ya Taasisi ya Utetezi wa Haki za Wanyama na Utunzaji wa Mazingira (ZSPCA), katika mashindano ya maadhimisho siku ya wanyama duniani yaliyofanyika Kibele, Wilaya ya Kusini Unguja.
Alisema mabadiliko hayo ya kisheria ni muhimu kwa vile inaonekana sheria zilizopo sasa haziwezi kukomesha jambo hilo na badala yake kunahitajika mikakati zaidi kusaidia kuwalinda wanyama na vuguvugu la mateso linalowakumba wanyama hasa Ngombe na Punda.
Aidha, aliitaka jamii kujenga mapenzi na wanyama kwani wao ni viumbe kama binadamu na pia wana hisia kama wengine.
Sambamba na hayo, alisema Jumuiya yao imeanzishwa kwa ajili ya kutetea haki za wanyama na uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo, pamoja na kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, haki za wanyama bado hazijapewa msukumo mkubwa kwa vile wengi wao wanaandamwa kwa vipigo na kutwishwa mizigo mizito, kupita kiasi.
Jumuiya ya Taasisi ya Utetezi wa wanyama na Utunzaji wa Mazingira imeanzishwa mwaka 2007 ambapo kwa mara ya pili maadhimisho ya siku hiyo na kauli mbiu ya mwaka huu inasema "MAISHA BILA UKATILI KWA WANYAMA INAWEZEKANA"
Monday, 4 October 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment