Maendeleo ya CCM kwa kila mtu - Mama Shein
Mwandishi Maalum – Zanzibar
2 OCTOBER 2010
MKE wa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi Mama Mwanamwema Shein, amesema amani na utulivu uliopo nchini ni matokeo ya utekelezaji wa sera nzuri za Chama cha Mapinduzi.
Mama Shein hayo alipokuwa akizungumza na kikundi cha SACCOS cha wavuvi wa Chaza wa wilaya ya mjini katika ukumbi wa EACROTENAL mjini Unguja.
Aliwaomba wanawake wa kikundi hicho kuichagua CCM katika uchaguzi mkuu ujao kwani ndio chama chenye uwezo na uhakika wa kuendeleza amani, umoja na mshikamano visiwani Zanzibar.
“Bila amani na utulivu akina mama tunahangaika…hata kazi zetu hizi za maendeleo za kuvua chaza hazifanyiki”, alisema Mama Shein.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanawake visiwani humo kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kwao kupata mikopo kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, akizungumza na akina mama wa Mpendaye, mjini Unguja Mama Shein alibainisha wazi kuwa serikali ya CCM iliyoko madarakani imefanya mengi na wala haibagui katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na hivyo kuwaomba waipigie kura CCM kwa maendeleo.
“Serikali ya CCM iliyoko madarakani imejenga barabara, maskuli, vituo vya afya, imeimarisha hospitali zetu. Watu wote wanapita kwenye barabara hizo, wanatibiwa kwenye vituo hivyo, watoto wanasoma kwenye skuli hizo. CCM haibagui, maendeleo ni kwa kila mtu…hivyo naomba mzitie kura nyingi kwa CCM,” alidokeza Mama Shein.
Monday, 4 October 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment