Mawaziri msitawaliwe upendeleo, itikadi - Said Soud
Na Lulua Salum, TSJ
MWENYEKETI wa Chama AFP, Said Soud Said amewashauri Mawaziri waliochaguliwa kuunda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, kuondosha upendeleo na itikadi za kisiasa katika kuijenga Zanzibar mpya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Soud alisema ili kuijenga Zanzibar mpya mawaziri hao wawe tayari kuwajibika katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti huyo aliyewania Urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu uliopita, alisema mawaziri hao wakiwajibika vyema na watendaji wao watakuwa kioo na hivyo wananchi wataweza kufikia ndoto ya matarajio kwa Serikali hiyo.
Alisema ni vyema wakaondosha mivutano kati yao na watendaji wa chini ambao watateuliwa na Rais, kwani kipindi kilichopita Wizara nyingi zilikuwa na matatizo ya watendaji na ndio sababu kubwa ya kuibuka kwa migogoro.
Aidha alimuomba Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, kufanya mabadiliko ya watendaji wake kwani wananchi wengi wameonekana kukosa imani nao.
Alisema watendaji wengi wa wizara hiyo wamekuwa hawajali maslahi ya wananchi na badala yake kuweka maslahi yao mbele.
Alisema licha ya serikali kuunda Mahakama ya Ardhi, lakini imeshindwa kutatua suluhisho la kuondoa matatizo yaliyopo na imeonekana kuzidisha matatizo na migogoro kwa wananchi hasa kisiwani Pemba.
Mwenyekiti huyo alimtaka waziri husika kuliangalia kwa kina tatizo hilo na kulitafutia njia mbadala ya kuliondosha ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya watendaji wake ili kuleta sura halisi ya Zanzibar mpya inayotakiwa na wananchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment