Bima Zanzibar kukusanya bilioni 10
Na Mwandishi wetu
Jumla ya shilingi bilioni kumi zinatarajiwa kukusanywa na Shirika la Bima la Zanzibar kwa mwaka huu ukilinganisha na shilingi bilioni 5 kwa miaka mitatu iliyopita.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar, Iddi Khamis Haji, katika hafla ya kuwaaga Wajumbe wa Bodi ya Shirika hilo ambao wamemaliza muda wao.
Mkurugenzi Iddi amesema kiwango hicho kimefanikiwa kutokana na kutekeleza kwa vitendo mikakati waliojipangia ya kuongeza mapato ya shirika hilo chini ya usimamizi wa Bodi iliyomaliza muda wake.
"Hali ya shirika linaendelea vizuri hadi sasa kutokana na kuongeza mapato ya shirika hilo zaidi" amesema.
Akizungumzia mikakati ya baadae ya shirika hilo Mkurugenzi Mkuu huyo amesema jengo la makao makuu ya bima Zanzibar linaloendelea kujengwa katika maeneo ya Maisara linatarajiwa kuwa tayari mapema mwakani na hadi sasa matengezo ya jengo hilo yamefikia asilimia 60.
Amesema jengo hilo likimalizika linatarajiwa kutumika kama ofisi pamoja na kulifanyia biashara kwa kukodisha kwa lengo la kuongeza mapato zaidi ya shirika hilo kwa siku zijazo.
Mbali na jengo hilo Khamis amesema shirika la bima la Zanzibar lipo mbioni kuanzisha bima inayoendana na misingi ya dini ya kiislamu ambapo huduma hiyo wanatarajiwa kuwa ni wa kwanza kuanzisha Tanzania kati ya makampuni 28 ya bima yaliyopo Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo aliyemaliza muda wake, Mohammed Fakih Mohammed, amesema Shirika la bima linatakiwa kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza ikiwemo ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo makampuni mbalimbali ya bima yatafungua matawi yake nchini.
Mbali na hilo pia amewataka kutilia mkazo zaidi kuimarisha huduma kanda ya Pwani Tanzania Bara kutokana na kuwa asilimia 70 hadi 80 ya mapato yote ya bima ya Zanzibar yanapatikana kutoka huko.
Bodi ya bima iliyomaliza muda wake ilichaguliwa mwaka 2007 ambapo kwa mujibu wa sheria inatakiwa kuka madarakani kwa muda wa miaka mitatu.
Tuesday, 30 November 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment