Monday, 29 November 2010

WACHACHE WAJITOKEZA UCHAGUZI MADIWANI.

Wachache wajitokeza uchaguzi Madiwani

CUF yanyakua Wadi zote 3 Pemba


IDADI ya watu waliojitokeza kupiga kura za udiwani katika wadi mbali mbali ambazo hazikuishiriki uchaguzi uliopita imepungua ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

Washiriki wa uchaguzi huo walikuwa wachache wakilinganishwa na waliojitokeza kwenye upigaji kura wa Oktoba 31, ambapo ulimchagua rais wa Zanzibar, Rais wa Muungano, wabunge na Wawakilishi.

Akizungumza na Mwandishi wetu aliyefika katika Kituo cha kupigia kura Sebleni wadi ya Sogea, Zahrani Juma, alisema idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura imezorota sana hata watu wanaokuja kupiga kura wamekuwa wakijitokeza kidogo kidogo .

‘’Idadi iko chini sana mpaka sasa mchana watu hata 100 hawafiki waliojitokeza kupiga kura,’’Alisisitiza Mkuu huyo.

Aidha alisema zoezi limekwenda vizuri na hakuna kasoro zozote zilizojitokeza zinazoashiria uvunjaji wa amani.

Nae Mkuu wa Kituo cha Mwembe Shauri, wadi ya Kwahani, Suhuba Daudi alisema zoezi la upigaji kura limeenda vizuri isipokuwa idadi ya wapigaji kura waliojitokeza ni ndogo.

Alisema mpaka muda huo wa mchana hakuna muangalizi yeyote aliyefika kuangalia mwenendo wa uchaguzi isipokuwa wagombea na makatibu wa vyama.

Nae Mkuu wa Kituo cha Miembeni Haji Makame Ussi,alisema zoezi limeenda vizuri na hakuna kasoro zozote zilizojitokeza za uvunjaji wa amani katika zoezi hilo .

Aidha alisema mwamko si mkubwa kwa watu waliojitokeza kupiga kura ikilinganishwa na Uchaguzi Mkuu.

Alisema wasimamizi waliofika katika kituo chake ni waangalizi wa ndani TEMCO.

Majimbo mengine yaliopiga kura za udiwani ni jimbo la Magomeni, Wadi ya Nyerere, jimbo la Mji Mkongwe, Wadi ya Mchangani, Jimbo la Makunduchi wadi ya Kajengwa,Jimbo la Bumbwini Wadi ya Mangapwani,kwa Upande wa Pemba Jimbo la Ziwani wadi ya Wara, Jimbo la Wawi Wadi ya Nga’mbwa, na Jimbo la Chake Chake Wadi ya Msingini.

WAKATI huo huo BAKARI MUSSA, Pemba anaripoti ZOEZI la upigaji kura za Udiwani katika Wadi tatu za Pemba, umefanyika vizuri ingawaje wapiga kura hawakuwa wengi katika vituo vya kupigia kura.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Chake Chake Pemba, Afisa Uchaguzi wilaya ya Chake Chake, Rashid Suleiman Omar, alisema vituo vimefunguliwa mapema na upigaji wa kura umeanza tokea saa 1.00 asubuhi na hakuna matatizo ambayo yalijitokeza katika zoezi hilo.

Alisema wapiga kura wengi wamekwenda Vituoni kwa ajili ya kupiga kura na kurejea majumbani mwao ingawaje wapiga kura hao wamekwenda mmoja mmoja kinyume na ilivyotarajiwa.

Aliendelea kusema kuwa kwa upande wa ZEC, vifaa vyote vya Uchaguzi walivipeleka mapema ili zoezi hilo liende kwa wakati, jambo ambalo limefanya uchaguzi huo kuanza kama ilivyopangwa na Tume.

Omar, alieleza kuwa baadhi ya Wapiga kura walikwenda mapema vituoni kupiga kura na mapema ili kuwahi shughuli zao walizojipangia na ndio baadhi ya vituo kukawa na watu kidogo.

Wadi ambazo zimefanya uchaguzi huo wa Madiwani baada ya hapo mwanzo kuwepo na matatizo ya kiutendaji ni, Wadi ya Wara, Ng’ambwa, Msingini na Uwandani, ambazo ni majimbo ya Wawi , Ziwani na Chake Chake Pemba.

No comments:

Post a Comment