Monday 29 November 2010

TINDWA AELEZA IMUHIMU WA BARAZA LA USAFIRISHAJI.

Tindwa aeleza umuhimu wa baraza la usafirishaji

Na Maryam Talib, Pemba

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, amewataka wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo kisiwani Pemba kuunga mkono uundwaji wa Baraza la usafirishaji, ambalo litawasaidia katika harakati zao za kibiashara.

Tindwa alisema hayo hoteli ya Clove Inn, Chake Chake alipokuwa akilizindua baraza la usafirishaji mizigo Zanzibar kwa upande wa kisiwa cha Pemba.

Alisema kuanzishwa kwa baraza hilo kutasaidia kuirejesha Zanzibar kuwa kituo muhimu cha kibiashara Afrika Mashariki na Kati.

Aidha alisema kuanziswa kwa baraza hilo, kutakuwa ni chachu ya kushuka bei kwa bidhaa mbali mbali zinazoingizwa nchini ambazo hivi sasa kwa kiasi wananchi wamekuwa wakizinunua kwa bei ya juu.

Alisema baraza hilo lina lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara sambamba na wasafirishaji mizigo yao, na kuwataka wafanyabiashara kulithamini baraza hilo.

Nae Mwenyekiti wa baraza hilo Salim Taufiq, alisema lengo la kuanzishwa baraza hilo ni kuwapa nafasi wasafirishaji kuwa na sauti moja katika kulinda maslahi yao.

“Hii itasaidia katika kusimamia kushuka gharama za usafirishaji kiasi ambacho hali hiyo ikiwa itatekelezwa kikamilifu na wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo itasababisha kila mmoja kuweza kumiliki anachotaka”, alisema Mwenyekiti huyo.

No comments:

Post a Comment