Tuesday, 30 November 2010

OLE WAO WANAOCHEZEA UMOJA WETU - MAALIM SEIF

Ole wao wanaochezea umoja wetu – Maalim Seif


Na Abdi Shamnah, Pemba

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amewaonya watu wanaochezea na kutia chokochoko umoja na mshikamano uliopo nchini.

Alisema umoja, amani na utulivu uliopo Zanzibar hivi sasa ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo amewataka Wazanzibari kutokuwa tayari kuruhusu mtu yeyote kuvunja au kutia doa umoja huo.

Katibu Mkuu huyo, alisema hayo katika kiwanja cha Tibirinzi Chake Chake Pemba, alipokuwa akizungumza na wananchi na wanachama wa CUF, ambapo pamoja na mambo mengine aliwashukuru kwa kushiriki kwenye zoezi zima la uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Maalim Seif aliwataka wananchi kutokubali kurejeshwa walikotoka na kutowapa nafasi watia chokochoko kwani umoja na mshikamano uliopo hivi sasa miongoni mwa wananchi ndio silaha pekee ya kufikia maendeleo ya haraka kiuchumi na kijamii.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Umoja wa Kitaifa chini ya Rais Ali Mohamed Shein na Makamu wawili wa Rais, itaendeleza mshikamano huo na kumuomba Mwenyezi Mungu aubariki milele.

Alieleza kuwa azma ya wananchi ya kuwa na Serikali ya umoja wa Kitaifa kama walivyothibitisha katika kura ya maoni imetimia baada ya vyama vikuu vya CCM na CUF kupata viti vinavyowiana katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31,2010.

Alifafanua kuwa matokeo ya kura za urais na mgao wa viti katika majimbo ni ushahidi tosha jinsi ya umuhimu wa kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Maalim Seif aliwashukuru wananchi wa kisiwa cha Pemba kwa kushiriki katika kampeni za amani na utulivu, kiasi ambacho mchakato huo umemalizika bila kuwepo ugomvi au matusi katika majukwaa.

Mapema katika risala ya Mikoa miwili ya Pemba, wanachama wa CUF walipaza sauti kuiomba Serikali kusambaza Mabwanashamba katika wilaya zote ili kukabiliana na tatizo kubwa linalojitokeza la uharibifu wa mazao mbali mbali katika mashamba ya wakulima.

Nae mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa alisisitiza haja ya wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuonya kuwa kamwe hakutokuwa na neema bila ya kila mmoja kujituma kwa kufanya kazi.

Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wananchi na viongozi wa ngazi mbali mbali wa chama hicho pia ulihudhuriwa na Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM Haji Omar Kheir, ambae alifuatana na ujumbe wa Makamu huyo kutoka Unguja.

Katika salamu zake kwa wanachama na wapenzi wa CUF waliohudhuria mkutano huo, mjumbe huyo ambae ni Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, aliwaahidi kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar kwa mashirikiano na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

No comments:

Post a Comment