Tuesday 30 November 2010

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI -- HAROUN

Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji - Haroun


Raya Hamad, Maelezo


WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman, amesema serikali ina nia thabiti na itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara wa visiwa hivi kwa maslahi ya wananchi.

Haroun alisema hayo jana huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja kwenye ufunguzi wa utanuzi wa hoteli ya La Gemma dell'Est, ambapo waziri huyo alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein.

Alisema, suala la kuishirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Zanzibar, limewekwa bayana na kupewa kipaumbele katika programu ya Mpango Mkuu wa Kukuza Uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar (MKUZA).

Kwenye mpango huo, amesema serikali imeweka mipango ya kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji pamoja na sekta binafsi kushirikishwa moja kwa moja katika uchangiaji wa uchumi wa Taifa.

"Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji ili sekta hiyo nayo iweze kuchangia uchumi wa Taifa kwa lengo la kuinua maisha ya Wazanzibari", alisema Waziri huyo.

Waziri huyo aliupongeza uongozi wa hoteli ya La Gemma, kwa upanuzi huo ambao una lengo la kuvutia watalii zaidi nchini ambao ni muhimu katika kuongeza pato la Taifa.

Alisema upanuzi huo ambao umegharimu dola milioni sita, ni mfano wa kuigwa kwa hoteli nyengine hapa nchini na kuitaka hoteli hiyo kuzidi kujitangaza na kutumia vivutio vya Zanzibar kwa lengo la kuongeza watalii.

Naye Murugenzi wa Kampuni ya RENCO, Paolo Chiaro alisema ataendelea kuitangaza Zanzibar kimataifa kuwa kituo muhimu cha utalii duniani.

Mkurugenzi huyo alisema kampuni hiyo pia ina mipango thabiti ya kuongeza ajira kwa wazalendo ili kupunguza tatizo la ajira.

No comments:

Post a Comment