Monday, 29 November 2010

CHUMBUNI WAMPONGEZA PERERA.

Chumbuni wampongeza PereiraNa Simai Tano, MUM

WANANCHI wa jimbo la Chumbuni Zanzibar jana walijitokeza kwenye Uwanja wa ndege wa Abeid Aamani Karume mjini hapa kumpokea mbunge wa jimbo lao akitokea mjini Dodoma.

Wananchi hao wakiwa wamevalia sare za Chama cha Mapinduzi walimpokea Mbunge huyo aliekuwa akitokea Dar es salaam, ambapo wiki iliopita aliapishwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Pereira ambae ni mbunge wa jimbo la Chumbuni katika Mkoa Mjini Magharibi, aliteuliwa kuwa miongoni mwa mawaziri wa baraza la mawaziri la Rais Kikwete aliloliteua wiki iliopita.

Wananchi wa jimbo hilo wakiwa na furaha walimvisha shada la maua mbunge huyo katika hafla iliyofanyika Uwanja wa ndege na kuongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa jimbo hilo, Juma Haji Juma.

Akizungumza na wapiga kura wake na wananchi wengine, Pereira

aliwataka wananchi hao kuachana na malumbano yasiokuwa na maana na kuvunja kambi zao ili kushughulikia maendeleo ya jimbo lao na serikali kwa jumla .

vile vile alisema watu wa jimbo lake wasiwe na wasi wasi juu ya kuteuliwa kwake kuwa naibu waziri wa fedha msimamo wake utakua pale pale kuleta maendeleo katika jimbo lake amewataka vijana wa jimbo lake kukaa pamoja na kutafakari ni kitu gani cha kuanza mwanzo katika ahadi alizozitoa za kuleta maendeleo ya jimboni kwao.

Aliwataka kuendelea kukiunga mkono chama cha Mapinduzi na pia kufanyakazi kwa juhudi popote walipo kama njia ya kuharakisha maendeleo ya ncjhi yao.

Aliwashukuru wananchi hao na kusema kwamba yeye yuko pamoja na wananchi na kusisitiza kwamba atatekeleza ahadi zake kwa wananchi wote kama alivyozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Mbunge Pereira Ame Silima hii ni mara yake ya kwanza kuwa mbunge, ingawa ameitumikia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu na katika nafasi kadha ikiwemo Maliasili Misitu, na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Biashara.

No comments:

Post a Comment