Thursday 11 November 2010

BALOZI AMINA SALUM ALI AMESEMA USHIRIKIANO ULIJENGWA NA VYAMA VYA CCM NA CUF UENDELEZWE.

Na Mwanajuma Abdi

MWAKILISHI wa kudumu wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa, Balozi Amina Salum Ali, amesema ushirikino mkubwa uliojengeka baina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa vyama vya siasa vya CCM na CUF uendelezwe baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Hayo aliyasema jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo wa mji wa Zanzibar.

Alisema hli ya ushirikiano inahitaji kudumishwa na kuendelezwa ili nchi iweze kupiga hatua za kimaendeleo, ambapo kwa muda miaka 13 Zanzibar ilikumbwa na misukosuko ya kisiasa.

Alieleza nchi ya Tanzania ikiwemo Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka huu umefanyika kwa amani na utulivu, ambapo mataifa mbali mbali duniani yamekuwa yakipongeza hatua hiyo pamoja na nchi za Afrika Mashariki.

Hata hivyo, aliwataka Wawakilishi wanawake wawe wabunifu katika kuhakikisha taifa linapata kasi ya maendeleo pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kutetea sheria za wanawake na watoto katika kupiga vita unyanyasaji na ukandamizaji.

Balozi Amina alisema Baraza la mwaka huu wanawake kutoka chama cha CCM na CUF kuwa na mwamko katika elimu, hivyo anatarajiwa kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika maendeleo ya nchi.

Mapema Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho aliwashukuru wajumbe hao kwa kumrejesha tena kuwatumikia katika shughuli hizo, aliwakumbusha kwamba Julai 31 mwaka huu wananchi walipiga kura ya maoni iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na waliowengi wameunga mkono.

Alisema ZEC iliandaa kura hiyo baada ya wawakilishi kupitisha mswaada wa kuundwa kwa Serikali hiyo baada ya uchaguzi mkuu, hivyo aliwashauri wailinde Serikali hiyo itayoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mahammed Shein kwa kuwateuwa mawaziri na manaibu.

Alieleza tukio lililofanyika jana linaumuhimu mkubwa kwa vile ndilo litalomuwezesha Dk. Shein kuchagua viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya Saba.

No comments:

Post a Comment