Tuesday, 30 November 2010

POLISI ZANZIBAR WAAGIZWA KUJIANDAA KUKABILI UHALIFU WA MITANDAO

Polisi Z'bar waagizwa kujiandaa kukabili uhalifu wa mitandao


Na Mwantanga Ame

JESHI la Polisi Zanzibar limetakiwa kuanza kujiandaa kwa namna litakavyoweza kupambana na uhalifu wa kimataifa kwa kutumia mitandao ya kompyuta na silaha nzito, ulioanza kushamiri duniani.

Waziri asiekuwa na Wizara Maalum, Machano Othman Said, alitoa ushauri huo jana wakati akifungua semina ya siku moja kwa maafisa wa Jeshi la Polisi wanaosimamia mradi wa ulinzi wa Polisi Jamii, iliyofanyika ukumbi wa Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.

Waziri huyo alisema uhalifu wa kutumia kompyuta na mitandao ya intaneti na silaha nzito ni mpya katika Afrika na sasa umeanza kujitokeza katika sehemu mbali mbali ikiwemo mataifa yanayoendelea.

Alisema suala kama hilo linahitaji kufanyiwa kazi kwa vile uchumi wa Zanzibar unategemea sana soko la utalii na katika hatua yoyote linaweza kuingia dosari endapo wahalifu watafanikiwa kulipenya.

Hata hivyo, alisema kitendo cha kupungua kwa matukio ya matumizi ya nguvu na silaha kumejenga taswira nzuri kwa wageni na kushauri jambo hilo lisimamiwe zaidi ili hata dosari ndogo ndogo ziweze kudhibitiwa.

Kutokana na mafanikio hayo, Waziri huyo alisema serikali itahakikisha inatoa mchango wake ili kulifanya Jeshi hilo liwe na uwezo mkubwa zaidi wa kuimarisha amani ya nchi kuwawezesha wananchi kushughulikia maendeleo bila ya kubughudhiwa.

Waziri Machano aliwataka watendaji hao kuendeleza ushirikiano na wananchi kwa kuieneza zaidi elimu ya Polisi jamii kwa kutumia vyombo vya habari.

Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alieleza Polisi kwa kiasi kikubwa inawapongeza wananchi kutokana na mchango wao mkubwa uliofanikisha

dhana ya Polisi jamii kukubalika kwa wananchi.

Semina hizo zinatarajiwa kufanyika katika maeneo mbali mbali kwa muda wa siku tano ndani ya vitengo vya jeshi hilo ambapo lengo lake ni kuhakikisha kunakuwepo fursa zaidi za mawasiliano kati ya wananchi na Polisi.

No comments:

Post a Comment