Thursday, 11 November 2010

WAJITOKEZA 103 WAPIMA VVU CHINI YA ABCZ.

103 wapima VVU chini ya ABCZ


Na Khamis Mohammed


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Mohammed Saleh Jidawi, amesema, Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za taasisi na mashirika mbalimbali katika vita dhidi ya maambukizi mapya ya vurusi vya ukimwi nchini.

Hayo aliyaeleza wakati akizindua upimaji wa virusi vinavyosababisha ukimwi hoeli ya Bwawani mjini hapa jana ikiwa ni siku maalum kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sehemu za kazi.

Alisema kwa kuthamini michango inayotolewa na taasisi hizo, Serikali itakuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo na kutoa ushirikiano katika vita hivyo vinavyoyakabili mataifa mbalimbali duniani.

Hivyo, Katibu huyo aliwataka wananchi kujitokeza mara kwa mara wakati zinapotekea fursa hizo kwa lengo la kutambua afya zao na kuweza kujikinga iwapo watakuwa hawajapata maambukizo hayo.

Aidha aliwataka wakuu wa taasisi kutilia mkazo juu ya upimaji afya kwa wafanyakazi wao sambamba na kuwapatia huduma za lazima iwapo watakuwa wamepata maambukizi.

"Ukimwi ni maradhi kama yalivyo mengine, tujitokeze kupima afya zetu ili tuweze kuishi tukijielewa tupo katika hali gani", alieleza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, Asha Abdalla, alisema, pamoja na kuwa hali ya maambukizi ya ukimwi hapa Zanzibar si ya kiwango cha juu, lakini ni vyema kwa wanajamii kuchukua kila tahadhari kuhakikisha haitumbukii katika janga hilo.

Jumla ya watu 133 walijitokeza kupima katika uhamasishaji huo wa upimaji wa virusi vya ukimwi kwa wafanyakazi wa taasisi za binafsi na makampuni hapa Zanzibar ambapo watu wawili waligundulika kupata maambukizi.

Hivi sasa Zanzibar inakisiwa kuwa na watu waliopata maambukizo ya virusi vya ukimwi zaidi ya 6,000.

Zoezi hilo la uhamasishaji wa upimaji wa virusi vya ukimwi liliendeshwa na Umoja wa Unaojihusisha na masuala ya ukimwi kwa sekta binafsi Zanzibar (ABCZ), ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Baraza la Biashara la Afrika Mashariki katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kila ifikapo Novemba 11.

No comments:

Post a Comment