Tuesday, 30 November 2010

MADRASAT TAQWA YATAKIWA KUZIKABILI CHANGAMOTO

Madrasat Taqwa yatakiwa kuzikabili changamoto


Na Masanja Mabula, Pemba


MWAKILISHI wa Shirika la Agakhan Foundation Zanzibar, Khamis Said ameuagiza uongozi wa Madrasat Taqwa ya Bubujiko wilaya ya Wete kisiwani Pemba, kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili madrasa hiyo ikiwemo kukamilisha banda la kusomea pamoja na kuwahimiza wazazi kulipa ada kwa wakati.

Akizungumza na Uongozi, wazazi na wanafunzi wa madrasa hiyo katika sherehe za siku ya Afya ya madrasa, alisema ni vyema uongozi huo ukashirikiana na wazazi ili kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa baadhi ya changamoto katika madrasa hiyo na kuacha tabia ya kusubiri wafadhili kuja kuwatatulia matatizo yao.

Alisema viongozi wa madrasa hiyo wanapaswa kutambua umuhimu wa afya, lishe na elimu kwa watoto wao, hivyo ni wajibu wao kutoa ushirikiano utakaoweza kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na walimu wa madrasa hiyo kuwapatia elimu bora ya maandalizi watoto kabla ya kuingia elimu ya msingi.

Aidha alifahamisha kuwa Shirika la Agakhan Foundation kanda ya Zanzibar, litaendelea kuzisaidia madrasa kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu ya kielimu pamoja na kuimarisha hali ya afya na lishe kwa wazazi na watoto.

Mapema Mratibu wa Zanzibar Madrasa Resource Centre Ofisi ya Pemba, Hassan Ali Bakar, alisema siku ya afya ya madrasa ni miongoni mwa mikakati ya Jumuiya ya ZMRC katika kutoa elimu ya afya na lishe kwa wazazi na wanajamii wa jamii mbali mbali za Zanzibar, sherehe ambazo hufanyika kila baada ya miezi mitatu katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa katika kusherekea siku hiyo , Jumuiya hualika wataalamu wa afya na lishe na kutoa mafunzo kwa wazazi na wanajamii kulingana na mahitaji ya jamii husika ambapo madaktari hupata fursa ya kuchunguza afya za watoto.

Katika sherehe hizo ambazo mgeni rasmi alikuwa ni Sheikh Khazal, alichagia mifuko kumi ya saruji ili kusaidia ujenzi wa madrasa hiyo na kuwataka wazazi kutilia umuhimu suala la afya na lishe katika makuzi ya watoto.

Kwa mwaka huu wa 2010, hapa Kisiwani Pemba, sherehe hizo zimefanyika kwa mara ya nne ambapo zaidi wa watoto 50 waliobahatika kuchunguza afya zao huku mtoto mmoja aliyepatikana kuwa na maradhi ya utapiamlo.

No comments:

Post a Comment