Monday, 29 November 2010

PEMBA WAPIGA KURA KWA MURUA.

Pemba wapiga kura kwa murua

Na Bakari Mussa, Pemba

ZOEZI la upigaji kura za Udiwani katika Wadi tatu za Pemba, umefanyika vizuri ingawaje wapiga kura hawakuwa wengi katika vituo vya kupigia kura.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Chake Chake Pemba, Afisa Uchaguzi wilaya ya Chake Chake, Rashid Suleiman Omar, alisema vituo vimefunguliwa mapema na upigaji wa kura umeanza tokea saa 1.00 asubuhi na hakuna matatizo ambayo yalijitokeza katika zoezi hilo.

Alisema wapiga kura wengi wamekwenda Vituoni kwa ajili ya kupiga kura na kurejea majumbani mwao ingawaje wapiga kura hao wamekwenda mmoja mmoja kinyume na ilivyotarajiwa.

Aliendelea kusema kuwa kwa upande wa ZEC, vifaa vyote vya Uchaguzi walivipeleka mapema ili zoezi hilo liende kwa wakati, jambo ambalo limefanya uchaguzi huo kuanza kama ilivyopangwa na Tume.

Omar, alieleza kuwa baadhi ya Wapiga kura walikwenda mapema vituoni kupiga kura na mapema ili kuwahi shughuli zao walizojipangia na ndio baadhi ya vituo kukawa na watu kidogo.

Wadi ambazo zimefanya uchaguzi huo wa Madiwani baada ya hapo mwanzo kuwepo na matatizo ya kiutendaji ni, Wadi ya Wara, Ng’ambwa, Msingini na Uwandani, ambazo ni majimbo ya Wawi , Ziwani na Chake Chake Pemba.

No comments:

Post a Comment