Wednesday, 1 December 2010

FAWE YASAIDIA ZAIDI YA 400 WENYE HALI NGUMU

FAWE yasaidia zaidi ya 400 wenyehali ngumuNa Suleiman Almas

JUMLA ya watoto 430, wamesaidiwa kuendelea na masomo na Jumuiya ya wanawake ya kusaidia watoto wa kike katika kukuza maendeleo kielimu (FAWE), baada ya kuonekana kuwa na hali ngumu kimaisha.

Miongoni mwa idadi hiyo 130, ni vijana wa kiume ambao wamebahatika kupatiwa msaada huo kupitia Taasisi hiyo iliyo msitari wa mbele kuwatetea na kuwainua watoto wa kike kielimu.

Akizungumza na gazeti hili, Mratibu wa FAWE, Asma Ismail, alifahamisha kuwa pamoja na Jumuiya hiyo kuwa na ukaribu mkubwa na watoto wa kike zinapotokea nafasi za msaada kwa vijana wa kiume hawasiti kuwasaidia.

Alisema nafasi hizo kutoka skuli 96, za Unguja na Pemba kwa watoto hao, ziliaza mwaka 2005 hadi 2011 kwa wanafunzi 300, wa kike kwa elimu ya msingi na kuendelea, mwaka 2008 mpaka 2010 ni kwawatoto wa kiume 130.

Aidha Asma, alieleza mafunzo mengine ambayo yametolewa na FAWE ni kuhusu masuala ya kijinsia ambapo jumla ya walimu 27, walipatiwa taaluma hiyo wakati walimu sita na wanafunzi 64, walipata mafunzo kama hayo kwa skuli ya Kijini.

Jumuiya hiyo ya (FAWE) katika kuhakikisha watoto wanapata elimu kama ilivyopangwa imetoa walezi 40 kwa Unguja na Pemba kupitia skuli ambazo wamo wanafunzi waliopatiwa msaada huo kuangalia mwenendo mzima wa watoto hao ikiwemo na mahudhurio.

FAWE ambayo ilianzishwa mwaka 1998 na kuzinduliwa rasmi kama Jumuiya isiyo ya Kiserikali mwaka 2001, tayari imeendesha mikutano 16 ya uhamasishaji jamii kuhusu elimu kwa mtoto wa kike.

No comments:

Post a Comment