Sunday, 17 July 2011

MIMBA, NDOA ZAENDELEA KUWAKOSESHA ELIMU WATOTO WA KIKE,

Mimba, ndoa zaendelea kuwakosesha elimu watoto wa kike

Na Mwanajuma Abdi
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imesema kesi 28 za wanafunzi kupata ujauzito na kesi 22 za ndoa zimeripotiwa katika mwaka 2010/2011.
Waziri wa Wizara hiyo, Ramadhan Abdalla Shaaban aliyasema hayo, ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio na mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Alisema kesi 28 za ujauzito zimeripotiwa, kati ya hizo kesi tatu ziliwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi, ambapo kesi 10 ziliweza kujadiliwa katika Ofisi ya Mrasjis wa elimu na wanafunzi wanane walikubali kuendelea na masomo, wawili walikataa, ambapo 18 hawakuhudhuria katika kikao cha majadiliano.
Aidha alieleza katika kipindi hiki kesi 22 za ndoa za wanafunzi ziliripotiwa na kati ya hizo kesi mbili ziliwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi.
Waziri Shaaban alifafanua kuwa, wanafunzi 24 wamefukuzwa skuli wakihusisha wanawake 22 na wanaume wawili kwa makosa mbali mbali, ambapo kwa mwaka 2011/2012 Kitengo cha Urajis kitaendelea kushughulikia kesi za ujauzito na ndoa za wanafunzi.
Alisema juhudi zitachukuliwa katika kupambana na mimba za utotoni, ndoa za mapema na madawa ya kulevya pamoja na kuelimisha stadi za maisha kwa walimu, wazee na wanafunzi katika skuli zote za Unguja na Pemba.
Aliongeza kusema kwamba, katika juhudi za kusimamia utaoji wa elimu katika skuli za sekondari katika mwaka wa feddha imekusudia kufungua skuli mpya 16 pamoja na kuongeza walimu wenye sifa hasa wa masomo ya sayansi, kuongeza idadi ya vitabu vya kusomea na vifaa vya maabara.
kizungumzia elimu ya msingi alieleza Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto duniani (UNICEF) na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika linakusudia kutoa mafunzo juu ya mbinu za kukomesha utumikishwaji wa watoto kama mpango wa kitaifa unavyoelekeza.
Alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wataendelea na mpango wa kutokomeza maradhi ya kichocho kwa watoto waliopo maskulini.
Hata hivyo, alifafanua mradi wa uhamasishaji wa walimu juu ya matumizi ya adhabu mbadala maskulini unaofadhiliwa na Shirika la Save the Children unaendelea vizuri na utekelezaji wake katika skuli 10 za majaribio zikiwemo sita za Unguja na nne za Pemba.
Alifahamisha kuwa, lengo kubwa la mradi huo ni kuwahamasisha walimu wa skuli, walimu wa vyuo vya kuran, walezi na wazazi kutumia adhabu mbadala badala ya kutoa adhabu zenye madhara kwa wanafunzi na watoto majumbani.
Alisema hiyo itasaidia kujenga uhusiano mzuri baina ya walimu na wanafunzi, wazee na watoto wao na jamii kwa ujumla, ambapo hadi sasa umewahamasisha walimu, kamati za skuli, masheha, Serikali za wanafunzi, wakaguzi, Maofisa wa Wilaya na Mikoa na walimu wa madrasa na vyuo vya kuran.
Alizitaja skuli zilizokuwepo katika majaribio ni pamoja na Regezamwendo, Kinyasini, Fujoni, Kisiwandui, Kitogani na Marumbi kwa Unguja na Pemba ni Pondeani, Ng'ombeni, Wingwi na Minungwini.
Alieleza mikakati yao ni kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa haki ya elimu iliyo bora kwa kuwajengea mazingira rafiki yanayomjali mtoto bila ya ubaguzi au vikwanzo.
Waziri Shaaban alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 aliomba Baraza liidhinishe matumizi ya Wizara hiyo shilingi 102,618,054,000, ambapo kati ya hizo shilingi 45,308,000,000 kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi 57,310,054,000 kwa kazi za maendeleo.

No comments:

Post a Comment