Mabadiliko makubwa Shirika la Meli
Bandari, Viwanja vya ndege kukusanya mabilioni
Na Halima Abdalla
WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad amesema Wizara yake inakusudia kufanya maamuzi ya kubadili meli zilizopo ambazo zimepitwa na wakati na kuziuza na kununua meli nyengine zitakazoweza kuhimili ushindani wa soko.
Alisema pia kutaanzishwa ajira ya mkataba kwa mabaharia wa meli zilizopo nchini pamoja na kukamilisha sheria ya uanzishwaji upya wa shirika la Meli na wakala.
Waziri Masoud alisema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na matumzi ya Wizara MiundoMbinu na Mawasiliano kwa mwaka 2011/2012 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar kinachoendelea.
Aidha, alisema kwa mwaka 2011/2012 Shirika la Bandari linategemea kuteremsha na kupakia kiasi cha tani 100,000 za mizigo mchanganyiko pamoja na makontena 30,000.
Alisema kwa upande wa miradi ya maendeleo shirika linatarajia kuendelea na uimarishaji wa huduma na rasilimali zake kwa kuimarisha miradi iliyoanzishwa mwaka wa fedha unaomalizika ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufanyia kazi bandarini na ununuzi wa taa za Solar kwa minara na maboya Unguja na Pemba.
Sambamba na hayo, alisema Shirika linatarajia kukusanya shilingi bilioni 9.3 katika kipindi cha Julai 2011 hadi Juni 2012 katika kutekeleza malengo hayo shirika, limepanga kutumia shilingi 6.5 billioni kwa kazi za kawaida.
Aidha, alisema kwa mwaka 2011/2012 Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kupitia Idara ya ujenzi na utunzaji barabara inakusudia kutekeleza na kusimamia miradi mbali mbali ya ujenzi wa Barabara iliyopangiwa.
Alisema Idara kupitia mfuko wa barabara itaendelea kuzitunza na kuzifanyia matengenezo barabara mbali mbali za mijini na vijijini Unguja na Pemba, ili zipitike muda wote kwa lengo la kuwarahisishia wananchi usafiri.
Aidha, alisema Idara ya usafiri na leseni katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012 itachukua hatua mbadala kuimarisha usalama barabarani ikiwemo kuendelea kuwapatia elimu watumiaji wa barabara na kuimarisha ukaguzi wa vyombo vya moto.
Alisema hatua pia zitachukuliwa kuhakikisha kuwa karakana kuu ya Unguja na sehemu ya mitambo Pemba zinaimarishwa kwa kupatiwa vifaa na wafanyakazi wenye ujuzi na teknolojia ya kisasa ya vyombo vya moto.
Alieleza kuwa mwaka 2011/2012 Idara ya usafiri na leseni inatarajia kukusanya jumla ya shilingi milioni 280,600,000 na inaombewa jumla ya shilingi milioni 370,000,000,kwa matumizi ya kazi za kawaida.
Sambamba na hayo, alisema katika kipindi cha mwaka 2011/2012 Mamlaka ya viwanja vya ndege inatarajia kukusanya shilingi bilioni 1,210 410,000 kutekeleza shughuli zake kama ilivyopangiwa.
Mamlaka jiyo imeombewa shilingi milioni 806,000,000 kwa ajili ya kazi za kawaida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi, Makame Mshimba Mbarouk, aliipongeza Wizara hiyo kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa barabara.
Alisema hiyo inajumuisha miradi ya Barabara mbali mbali inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo na Serikali pamoja na barabara zinazofanyiwa matengenezo chini ya usimamizi wa Idara ya ujenzi na utunzaji wa barabara kwa fedha kutoka mfuko wa barabara.
Mshimba alisema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Alisema bandari zimekuwa zikikusanya mapato kutokana na vyanzo mbali mbali inayopitishwa katika bandari hizo, lakini muhimu zaidi zimekuwa mlango unaotumika kama chanzo cha kukusanyia mapato kwa Idara nyengine kama vile Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).
No comments:
Post a Comment