Mvuvi ahofiwa kupotea baharini Pemba
Na Zuhra Msabah, Pemba
MTU mmoja mwanamme, hajulikani aliko akisadikiwa kupotea baharini alikowenda kuvua katika kijiji cha Tumbe wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, alimtaja mtu huyo kuwa Mbarouk Faki Hamad (49) mkaazi wa Tumbe Shangani, ambaye aliondoka Julai 12 mwaka huu kwenda kuvua uvuvi wa madema kwa kutumia dau.
Kamanda Bugi alifahamisha kuwa Hamad aliondoka bandarini Tumbe saa 1:00 asubuhi ya siku hiyo lakini hadi ilipofika jioni hakuwa amerejea.
Kufuatia hali hiyo, Bugi alisema ndipo wananchi walipoamua kwenda kumtafuta, lakini kwa mshangao, walikikuta chombo chake kikielea bila yeye mwenyewe kuonekana.
Hadi wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana mvuvi huyo alikuwa hajaonekana wala kupata fununu zinazomuhusu na kueleza jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Kamanda huyo alisisitiza kwa wavuvi kuacha tabia ya kwenda baharini mtu mmoja peke yake, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa endapo kutatokea jambo lolote lisilotarajiwa.
Friday, 15 July 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment