Saturday 23 July 2011

TANI 140 ZA NERICA KUSAMBAZWA.

Tani 140 za NERICA kusambazwa

Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI imesema inakusudia kusambaza wastani tani 140 za mbegu mpya ya mpunga wa juu ya NERICA kwa wakulima wa Unguja na Pemba na kudhibiti uingizwaji na matumizi wa msumeno wa moto nchini.
Katibu mkuu wa wizara Kilimo na Maliasili, Affan Othman Maalim alieleza hayo jana huko ofisini kwake Darajani mjini hapa kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mansour Yussuf Himid alipokuwa akitia mwelekeo wa bajeti ya wizara mbele ya waandishi wa habari.
Alisema tani hizo za mbegu hiyo mpya ya NERICA zitasambwa kwa wakulima mbegu ambayo inaweza kuzalishwa katika eneo lisilo na maji mengi, huku pia kanuni zikiwa zimeshaandaliwa kuhakikisha misumeno ya moto inapigwa marufuku nchini ikiwa ni hatua ya kudhibiti ukataji ovyo wa miti.
Alisema kilimo cha mpunga cha mabondeni kwa mbegu BKN, super India, TXD 88 na TXD 306 zitaongezwa upatikanaji wake kutoka tani 124 kwa mwaka uliopita na kufikia tani 215 kwa mwaka 2011/2012.
Alieleza usambazaji wa mbegu huo utakuwa unakwenda sambamba na kuongezeka kwa zana za kisasa za kilimo kama matrekta, majembe ya kulimia na kuburugia, power tillers, seed drillers, mini combine harvestors, rice reappers na threshers, ambapo malengo hayo ni kwa ajili ya kufikia kauli mbiu ya Mapinduzi ya Kilimo.
Alisema dunia hivi sasa imekabiliwa na hali ya upungufu mkubwa wa chakula na tishio la njaa, hali hiyo inasababisha upungufu wa uzalishaji wa nafaka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa na kupanda kwa gharama za bei za mafuta, hivyo kunakuwepo ushindaji mkubwa wa chakula katika masoko ya kimataifa.
Alifahamisha kuwa wizara imeazimia kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua kwa kushirikiana na wahisani kutoka KOICA, USAID, TASAF na JICA katika kufanikisha hilo, pamoja na nguvu zitaendelea katika utafutaji wa mitego ya nzi wanaoharibu matunda.
Aidha alifahamisha kuwa, wizara hiyo imepania kuimarisha mkakati maalum wa uendelezaji wa kilimo cha matunda na viungo kwa kuongeza uzalishaji wa kibiashara ni pamoja na karafuu, pilipili kichaa, manjano, mdalasini, vanilla, pilipili manga na mchaichai, ambapo mvuje, mrehani, hina, zingifuri, tangawizi, hiliki na kungumanga zitaimarishwa kwa ajili ya utafiti, mafunzo na matumizi ya ndani, ikiwemo maonyesho ya watalii.
Alisema katika kikabiliana na hali hiyo Wizara imepanga kuzalisha miche milioni moja ya viuongo, matunda, misitu ya mapambo, ikiwemo ya zao la karafuu ili kuliongezea nguvu kwa vile linasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza pato la uchumi wa taifa.
Katibu Mkuu Affan aliongeza kwamba, kilimo cha mazao ya juu nacho kimepewa kipao mbele katika uzalishaji huo pamoja na kuendeleza kufanya utafiti katika mazao mbali mbali hasa ya chakula kama muhogo, viazi, migomba, mpunga na mboga mboga.
Aidha alieleza wataendeleza matumizi ya mbegu bora na utaalamu kwa wakulima wengi kwa mazao mbali mbali kupitia skuli za wakulima ili kuongeza uzalishaji pamoja na kusambaza mbegu mpya za muhogo zenye kustahamili maradhi na wadudu, ambazo zimezalishwa Kizimbani, Machui, Mahonda na Kama kwa ajili ya kuwapatia wakulima.
Alisisitiza kwamba kilimo cha maweni kitaendelezwa uzalishaji wa mbaazi, mtama, uwele, fiwi, viazi vikuu na pilipili hoho, ambazo ni mazao makuu ya ukanda wa maweni, ambapo itawahamasisha wakulima matumizi endelevu ya rasilimali za ardhi na maji katika kuendeleza kilimo hicho bila ya kuathiri mazingira na maliasili zilizopo.
Alisema bajeti hiyo inakusudia kujenga masoko wilayani yatayotoa huduma za uhifadhi wa bidhaa zinazoharibika, ujenzi wa viwanda viwili vya kuzalisha barafu, kuanzisha mfumo wa utoaji wa huduma za kifedha vijijini na kuimarisha vikundi vya wajasiriamali katika usindikaji na usarifu wa bidhaa za kilimo.
Alieleza sekta ya kilimo inachangia asilimia 24 ya pato la taifa na inakadiriwa kuwa asilimia 75 ya wananchi wanategemea sekta hiyo katika chanzo cha ajira na mapato yao.

No comments:

Post a Comment