Saturday, 23 July 2011

MAALIM SEIF VIWANGO VYA KODI KUANGALIWA UPYA.

Maalim Seif: viwango vya kodi kungaliwa upya

Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema serikali itaangalia viwango vya kodi vinavyotozwa kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini.
Alisema anaamini viwango vikubwa vya kodi havisaidii, bali ni njia ya kuwaumiza watu na kuwafanya wafanyabiashara wakimbie, sambamba na kuwanufaisha baadhi ya watu wachache kutoka taasisi zinazosimamia makusanyo hayo.
Maalim Seif amesema hayo jana ofisini kwake Migombani, alipokuwa na mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na Wakulima Zanzibar, waliofika kujitambulisha na kubadilishana mawazo.
Alisema kuna umuhimu wa viwango vya kodi vinavyotozwa kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini kuangaliwa upya, ili Zanzibar irejeshe hadhi yake ya kuwa kituo muhimu cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema iwapo viwango vya kodi vitapungua, ni wazi kuwa bidhaa nyingi zaidi na zilizo bora zitaingia nchini na kuuzwa kwa bei nafuu, hivyo kufungua milango kwa wafanyabiashara wa ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika kuja Zanzibar, badala ya kwenda ughaibuni.
“Iwapo Zanzibar itafanikiwa kuleta kwa wingi bidhaa zilizo bora na kuziuza kwa bei nafuu, hakutakuwa na sababu kwa wafanyabiashara kutoka Malawi,Kenya, Msumbuji na kwengineko kwenda Dubai au Thailand”, alisema.
Akizungumzia hoja ya kubinafsishwa kwa zao la karafuu kwa lengo la kumnufaisha zaidi mkulima, Maalim Seif alisema serikali inaifanyiakazi hoja hiyo, ikitilia maanani uepukaji wa matatizo mbali mbali yanayoweza kujitokeza.
Alisema moja mifano inayoangaliwa kwa karibu na serikali ni ule wa bidhaa ya mwani, ambapo umeonekana kuwanufaisha zaidi mawakala na wafanyabiashara wakubwa huku ukiwaacha wakulima wakiendelea kusumbuka kutokana na kiwango kidogo cha bei ya bidhaa hiyo, ikilinganishwa na linavyouzwa katioka soko la Dunia.
Alisema utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa matajiri wamekuwa wakiwakandamiza wakulima kutokana na bei ndogo wanayowalipa ikilinganishwa na faida waipatayo.
Maalim Seif alisema serikali iko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wazalendo wenye uwezo wa kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo, hivyo aliwataka wanachama wa jumuiya hiyo kueleza azma zao.
Alitumia fursa hiyo kuwathibitishia wanachama hao uwezekano wa wajumbe wake kushirikishwa katika Bodi mbali mbali zinazoundwa na serikali, hususan katika sekta zinazohusika na biashara au uchumi.
Aidha aliwahakikishia viongozi hao uwezekano wa kuhusishwa katika mijadala mbali mbali ya kisheria katika hatua za maandalizi ya awali (draft) kwa lengo la kupatikana mawazo yao.
Alibainisha kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, kwa mujibu wa sheria zilizopo ndie mwenye jukumu la kuzingatia iwapo upo uwezekano wa wanajumuiya hiyo kuhusishwa katika mijadala ngazi za kamati.
Mapema Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na Wakulima Zanzibar, Mbarouk Omar Mohamed, alisema hali ya amani na utulivu iliopo hivi sasa nchini, imeifanya Zanzibar kuwa mahala pazuri zaidi pa kuishi na kuwa kichocheo katika kukuza biashara.
Alisema Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, wana fursa nzuri ya kuwekeza katika miradi mbali mbali na kuendeleza biashara, kwa maslahi na maendeleo ya nchi.
Alishauri Serikali kupunguza viwango vyake vya kodi, hususan katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, hatua aliyosema itaifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha kibiashara na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka mataifa mbali mbali jirani kuja kununua bidhaa hizo badala ya kukimbilia nchi za mbali.
Alitoa mfano wa nchi kama Dubai na kusema imefikia maendeleo makubwa ya kibiashara kutokana na mfumo wa ulipaji kodi nafuu, unaowawezesha wafanyabiashara kutoka sehemu mbali mbali Duniani, ikiwemo Zanzibar kukimbilia huko.

1 comment:

  1. ASANTE SANA MAALIM SEIF. SISI WAZANZIBARI AMBAO TUKO NJE TUNATAKA SANA KUWEKEZA NYUMBANI,LAKINI TUMESHINDWA KWANI SASA HIVI HAKUNA SERIKALI BALI KUNA KIKUNDI CHA CRIMINALS HAPO.KAMA MUNGU ATATUJALIA TUONGOZE NCHI YETU SISI WENYEWE BASI TUKO NYUMA YAKO KWA LOLOTE, INSHAALAAH....AMEEN.

    ReplyDelete