Friday, 15 July 2011

VIJANA EPUKENI MAKUNDI YASIOPENDA KUJIELIMISHA - MWAKILISHI.

Vijana epukeni makundi yasiopenda kujielimisha-Mwakilishi

Na Khamisuu Abdalla
VIJANA wameshauriwa kujiepusha na makundi yenye mitizamo ya kubeza elimu na kujiingiza katika makundi yasiokuwa na maana ambayo wakati wote yanafikiria kutumia njia za mkato katika kuendesha maisha yao.
Akizungumza na wajumbe wa kituo cha (Suza American Conner) katika kuadhimisha miaka mitano ya kituo hicho, Mwakilishi wa Amani, Fatma Mbarouk Said, alisema huu ni muda muafaka kwa vijana kujihusisha na masomo badala ya kuzurura mitaani.
Alisema vitendo viovu ambavyo sehemu kubwa ya vijana wameviweka mbele haitawasaidia kuwaondoshea matatizo badala yake vinawaingiza kwenye vitendo viovu kila kukicha.
Aidha, mwakilishi huyo alisema pamoja na huduma ya Intaneti inayotolewa na kituo hicho lakini itakuwa haiwasaidii vijana hao kwa kuitumia kinyume na dhamira iliyokusudiwa.
Hata hivyo, Mwakilishi Fatma alisema kuwa amefurahishwa na uendeshaji wa kituo hicho kwa kuhusisha somo la kujifunza kingereza (American Corner English Club) na kuwataka kuitumia fursa hiyo hasa vijana wa kike ambao ni wachache kwenye klabu hiyo ikilinganishwa na vijana wa kiume.
Kiongozi wa klabu hiyo, Mbarouk Kheir Othman alisema kituo hicho kimeweza kuendesha programu tofauti za kuendesha maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na taasisi zisizokuwa za kiserikali kama vile Ukimwi, dawa ya kulevya, Mtoto wa Afrika, Siku ya wanawake, Siku ya Wafanyakazi na pia kushirikiana na serikali na taasisi mbali mbali kuendesha programu hizo.
Alisema umefika wakati Baraza la Wawakilishi kutumia kituo hicho katika kuelimisha juu ya masuala ya uendeshaji wa shughuli za Baraza ili kituo hicho kichukue elimu hiyo na kusambaza kwa wananchi wa kawaida.
American Corner ni kituo kilichofadhiliwa na Wamarekani chini ya chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kilichofunguliwa Julai 13, 2006 na aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Michael Retzer.
Ujumbe wa mwaka huu kutoka kituo hicho "American Conrner ni Sehemu sahihi kwa kupata habari kuhusu Marekani".

No comments:

Post a Comment