Friday, 15 July 2011

KAMPUNI MPYA YAJITOKEZA KUNUNUA MWANI KUSINI.

Kampuni mpya yajitokeza kununua mwani Kusini

Na Ameir Khalid
MKUU wa Wilaya ya Kusini Haji Makungu Mgongo amezishauri Kampuni zinazonunua mswani kujali maslahi wakulima wa zao hilo, kutokana na kazi nzito wanayoifanya.
Alisema zipo kampuni zinazojitokez kwa wakulima kununua zao hilo na kuangaza bei ya chini ya ununuzi wakiwa na lengo la kujinufaisha zaidi wakisahau ugumu wa kazi hiyo unaowakabili wakulima.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na uongozi wa kampuni ya Shopping Center, pamoja na wakulima wa zao hilo wakati wa kuitambulisha kampuni hiyo kwa wakulima.
''Huu ni wakati mzuri kwa wakulima kunufaika na jasho lao kwani endapo zitakuwepo kampuni nyingi za kununua mwani kila mkulima atakwenda anakotaka ambako anaona kuna maslahi na yeye''alisema.
Aliongeza kusema kuwa wilaya yake ipo tayari kukaribisha kampuni yoyote ambayo itakuwa miongoni mwa kampuni zitakazonunua zao hilo, baada ya kupata vibali na taratibu za biashara hiyo.
Mkurugenzi wa kampuni ya mwani shopping center Omar Haji, alisema kampuni yake imeamua kununua mwani kwa wilaya nzima ya Kusini kwa lengo la kuongeza kipato kwa wakulima wa zao hilo.
Alisema kampuni yake itajikurubisha zaidi kwa wakulima ili iweze kujua matatizo yanayowakabili, pamoja na kushirikiana nao ili mafanikio ya pande zote mbili yaweze kupatikana.
Aidha ameahidi kutoa vifaa mbali mbali ambavyo zinatumika katika kilimo cha zao hilo, bila ya malipo kwa lengo la kuwafanya wakulima hao wazidishe kulima kwa wingi.
Katika mkutano huo wakulima hao walielezea matatizo mbali mbali yanayowakabili katika kilimo cha mwani, ambapo waliomba zipatiwe ufumbuzi wake kwa lengo la kuongeza tija zaidi kwa zao hilo.
Miongoni mwa matatizo hayo ni ukosefu wa vifaa vya kulimia ikiwemo kamba, jambo linalochangia kurudisha nyuma utendaji wao.

No comments:

Post a Comment