Thursday, 14 July 2011

MAMIA WAMZIKA MZEE WA ASP.


Mamia wamzika mzee wa ASP
Na Mwandishi wetu
MAMIA ya wananchi wa Zanzibar na vitongoji vyake, jana walihudhuria maziko ya Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, mzee Masoud Sururu, aliyezikwa kijijini kwao Kiombamvua, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.
Maziko hayo yaliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Rais (Mstaafu) wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume.
Aidha, viongozi wengine wa chama na serikali walihudhuria ikiwa ni  pamoja na Makamu wa Pili  Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi (OMPR),  Mohamed Aboud Mohamed, baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM   na viongozi mbali mbali wa CCM  wa Mikoa mitatu ya Unguja.
Marehemu Sururu (89), alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) - Lugalo, mjini Dar es Salaam, baada ya kuugua maradhi ya kiharusi  kwa muda mfupi.
Wakati wa harakati za siasa, marehemu Sururu, alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa ASP katika miaka 1957, ambapo alibahatika kushika nyadhifa kadhaa ndani ya chama na serikali ikiwemo Mwenyekiti wa Tawi la ASP Mangapwani na Jimbo la Bumbwini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ASP na CCM, Ubunge pamoja na Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, wadhifa alioushikilia hadi kufariki kwake.
Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa mshituko, huzuni na masikitiko makubwa  taarifa ya kifo cha mzee Sururu, kwani kimekuja wakati huu chama hicho kikiwa  kimo katika harakati za kuleta mageuzi ya kiuongozi na Kiutendaji, ambapo hekima, busara na mchango wake, ulikuwa bado unahitajika katika kukijenga na kukiimarisha.
Hivyo, CCM imesema daima itamkumbuka marehemu Sururu, kutokana na ujasiri, uadilifu, ukaribu wake na watu wa rika na jinsia zote na kubwa zaidi alikuwa ni miongoni mwa wana CCM walioadiriki kutoa ushauri, nasaha, maelekezo katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi sio tu kwa maslahi ya chama, bali pia kwa taifa na wananchi wake.
Chama Cha Mapinduzi kimesema kinaungana na wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu wa mzee Sururu hasa katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na kwamba kinawaomba wawe na moyo wa subra kwa kuondokewa na mpendwa wa huyo.
Marehemu mzee Masoud Sururu Jumanne, ameacha vizuka wawili , watoto 14 na wajukuu kadhaa.
 Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema Peponi, Amiin.


No comments:

Post a Comment