Ofisi ya Mufti kuzindua kampeni usafishaji misikiti leo
Na Asya Hassan
OFISI ya Mufti wa Zanzibar kwa kushirikiana na kikundi cha vijana wa usafishaji Misikiti (AL-ISLAM MOSQUES CLEANING GROUP) leo kinatarajia kuzindua rasmi shughuli za usafishaji misikiti katika Wilaya ya Mjini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga kwa waandishi wa habari, ofisi yake imeamua kuwakusanya vijana waliojitolea kufanya usafi katika nyumba hizo za Mwenyezi Mungu.
Aidha, alisema Ofisi hiyo imefikia uamuzi wa kuanzisha kikundi hicho baada ya uchunguzi uliofanywa kubaini kwamba misikiti mingi na hasa sehemu ya vyoo kuonekana vichafu na kuhitaji kusafishwa.
Soraga alisema uzinduzi wa kazi hiyo unategemewa kufanyika leo asubuhi katika msikiti Mkuu wa Mwembe Shauri ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji Khamis.
Alifahamisha kuwa wakati shughili hiyo ikizinduliwa misikiti ya Gongoni,Nambari,Mabati,Mkuti na msikiti wa Sheikh Nassor Bachu wa Kikwajuni tayari imeshafanyiwa usafi na kikundi hicho.
Aidha Katibu wa Mufti alitoa wito kwa waumini mbali mbali kukiunga mkono kikundi hicho kwa kusaidia kuchangia vifaa mbali mbali vya usafishaji ili kufanikisha shughuli hiyo muhimu.
No comments:
Post a Comment