Saturday, 23 July 2011

MAPATO BAHARI KUU YAZUA MJADALA BARAZANI.

Mapato bahari kuu yazua mjadala Barazani

Mwakilishi asema ni kero nyengine ya Muungano
Na Mwantanga Ame
MWAKILISHI wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu ameibua tuhuma nzito juu ya Zanzibar kukoseshwa haki yake katika Muuungano ya mapato yatokanayo na leseni uvuvi wa bahari kuu.
Mwakilishi huyo aliibua hoja hiyo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka wa fedha 2011/2012 iliyowasilisha na waziri wa wizara hiyo Said Ali Mbarouk.
Jussa alimtaka waziri huyo kuliangalia vyema suala la fedha za leseni katika bahari kuu kwani Zanzibar inakoseshwa mapato yake na hawaoni kama serikali ya Muungano ina nia ya kushirikiana na SMZ juu ya mapato ya mgawano wa fedha zinAzokusanywa katika uvuvi wa bahari kuu.
Alisema sheria ya makubaliano juu ya mgawano wa mapato ya uvuvi wa bahari kuu yanataka Zanzibar kupewa asilimia 40 na bara asilimia 60 lakini hali iliyopo ni kwamba hiyo asilimia 40 Zanzibar haipewi.
Akifafanua kauli yake alisema katika kikao cha mwezi Juni 15, 2011, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo wa Tanzania, Benedict Ole Nangoro, akijibu Mbunge wa viti maalum Thuwaiba Idrisa Muhammed ambaye alitaka kujua kiasi gani na Zanzibar imeweza kufaidika na fedha za magao wa lesini za bahari kuu ambapo Naibu huyo alijibu fedha walizokusanywa na sio mgao wa Zanzibar
Alisema Naibu huyo aliliambia Bunge hilo kuwa kwa mwaka 2010/ 2011, meli ambazo zilivua baada ya kupatiwa leseni zilikuwa ni 71 na mapato yaliopatikana yalikuwa dola za kimarekani 2,074,000.
Alisema inasikitisha kuona mapato ya Zanzibar katika suala hilo imekuwa haipatiwi huku serikali ikiwa inatoa mchango wake wa kujenga jengo la Makao Makuu ya uvuvi wa bahari kuu huko Fumba.
Mwakilishi huyo anayechachafya Barazani alisema ipo haja ya wizara hiyo kuanza kufanya uchunguzi kwa kutafuta ni kwanini mgao uliotakiwa kupatikana kwa uvuvi wa bahari kuu mapato hayakufikishwa Zanzibar.
Alisema ni lazima serikali iliangalie hilo kwa vile Waziri wa wizara hiyo amekuwa akilalamikia ukosefu wa fedha kwa ajili ya utoaji wa huduma za baadhi ya ofisi kuwa na mchango mdogo huku kukiwa na fedha ambazo zingeweza kusaidia kukabiliana na changamoto za wizara hiyo.
Alisema tatizo hilo ni muendelezo wa vitendo vya serikali ya Muungano katika mambo ya mgawano wa mapato jambo ambalo hapo awali lilielezwa kuwa limeshapata ufumbuzi katika vikao vya kero za Muungano.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Matemwe, Abdi Mosi Kombo, alisema ipo haja kwa wizara hiyo kuwaandalia mazingira mazuri ya kuwapatia vifaa vya kisasa wavuvi wa eneo ili kazi yao hiyo iweze kuwafaidisha kimapato.
Nae Mwakilishi wa Kojani Hassan Hamad Omar, alisema ipo haja ya serikali kuliangalia suala la baadhi ya wavuvi wanaoenda kuvua Tanzania bara kutozeshwa kodi ya leseni ya shilingi 20,000 wakati wanaotoka bara kuja Zanzibar hawatozwi fedha hizo.
Mwakilishi wa Mkoani Abdalla Mohammed Ali, akitoa mchango wake alisema ipo haja kwa serikali ikaona inaimarisha sekta ya mifugo kwa kuwapatia wafugaji ng’ombe wa kisasa kwa mkopo kwani baadhi ya wafugaji hawana uwezo wa kununua mifugo hiyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Amaan, Fatma Mbarouk Said, alisema ipo haja kwa serikali ikawaangalia vijana ambao hivi sasa wanajishughulisha na ajira za Punda na ng’ombe kwa kuwapatia kazi ikiwa ni hatua itayowawezesha kuacha kuwatumia wanyama hao vibaya.
Nae Mwakilishi wa Mkwajuni Mbarouk Wadi Mussa Mtando, ameitishia kuzuiya bajeti hiyo ikiwa Wizara hiyo itashindwa kump maelezo juu ya gari lililonunuliwa kwa ajili ya mradi MACEMPU iliyokuwa ikitumiwa na Mkurugenzi wa Uvuvi ambayo hivi sasa haijulikani ilipo.
Wawakilishi wengine waliipongeza Wizara hiyo juu ya utekelezaji wa dhamira yake ya kuinua sekta ya uvuvi wa bahari kwa kufikiria kutoa boti kwa kila Wilaya zitazowawezesha wavuvi wapatao 20 kuvua bahari kuu.

No comments:

Post a Comment