Monday 18 July 2011

BALOZI SEIF VIJANA ACHENI KUKAA VIJIWENI KUTEGEMEA MJOMBA,

Balozi Seif: Vijana acheni kukaa vijiweni kutegemea 'mjomba'

Awahamasisha kufanya kazi za kujitolea
Na Aboud Mahmoud
VIJANA nchini wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi za kujitolea zenye manufaa kwao na Taifa.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi,wakati wa uzinduzi wa Kampeni endelevu ya usafi wa Mazingira iliyoandaliwa na Jumuiya isiyo ya Kiserikali ya ZASOSE katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema vijana wanapaswa kufahamu kwamba Wazanzibari na Watanzania lazima wafanye kazi wenyewe na kuacha tabia ya kudhania kuna mtu atakuja kuwafanyia kazi,
"Nataka niwape wasia aliotuachia Mzee Abeid Amani Karume unaosema lazima mfahamu kwamba sisi Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla hatuna mjomba wa kuja kutufanyia kila kitu,"alifafanua.
Balozi Seif alitoa historia ya kufanya kazi za kujitolea iliyofanyika miaka mingi na kuweza kujipatia umaarufu ni pamoja na ujenzi wa nyumba za maendeleo, Unguja na Pemba, Ujenzi wa uwanja wa Amaan ,ujenzi wa barabara mbali mbali, skuli na mambo mbali ambayo yameweza kuleta maendeleo makubwa ya nchi.
Alieleza kuwa kwa upande wa kilimo, vijana walianzisha makambi ya kilimo sehemu mbali mbali ikiwemo Bambi na sehemu nyenginezo na Unguja na Pemba, ambapo kwa sasa vijana wengi walioshiriki wamekuwa wakulima wa kupigiwa mfano.
Alifahamisha kuwa hakuna shughuli za maendeleo zilizofanyika visiwani Zanzibar bila ya nguvu za vijana ambapo kwa pamoja waliamua kujitolea.
Balozi Seif alichukuwa nafasi hiyo kuwapongeza vijana na hasa Jumuiya ya ZASOSE kwa kufanya uamuzi wa kuanzisha kampeni ya usafi unaotokana na kuguswa na tamko la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein lililosema kuwa hali ya Mji wa Zanzibar hairidhishi.
"Napenda kuwapongeza vijana mbali mbali mlioshiriki katika kampeni hii pamoja na Jumuiya ya ZASOSE kutokana na kufanya uamuzi wa kuanzisha kampeni hii inatokana na kuguswa na tamko la Rais,"alifahamisha.
Akisoma risala ya Jumuiya ya ZASOSE, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Shaka Hamdu Shaka, alisema kuwa lengo kuu la kuanzisha Jumuiya hiyo ni kusimamia, kuhakikisha na kutoa muamko kwa vijana na jamii juu ya suala la usafi na uhifadhi wa mazingira.
Katika uzinduzi huo, Jumla ya shilingi milioni 2,600,000 zilikusanywa kwa ajili ya kuchangia Jumuiya hiyo huku wengine waliahidi kutoa jumla ya shilingi milioni 5,555,000.
Miongoni mwa waliochangia ni Balozi Seif Ali Iddi (Milioni moja) na bado milioni moja na nusu, Mohammed Raza (Milioni moja) na Mwakilishi Mgeni Hassan Juma (500,000).
Wengine ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Sira Ubwa Mamboya (Milioni moja) na Mwakilishi wa Kikwajuni, Mahmoud Mohammed Mussa (300,000).

No comments:

Post a Comment