Monday 18 July 2011

VITA YA UKIMWI KUELEKEZWA ZAIDI KWA MAKUNDI HATARISHI.

Vita ya UKIMWI kuelekezwa zaidi kwa makundi hatarishi

Na Mwandishi wetu
MKAKATI wa pili wa kukabiliana na ukimwi (MPIKU II) utatoa kipaumbele zaidi kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (MSM),watu wanaofaya biashara ya ngono (CSW) na watumiaji wa dawa za kulevya, hasa wanaotumia sindano (IDU).
Kwa mujibu wa sheria za Zanzibar ni marufuku mtu kushiriki mapenzi ya jinsia moja na kufanya biashara ya kuuza mwili wake.
Makundi mengine yanayolengwa ni wanafunzi wa vyuo vya mafunzo na jamii kwa ujumla.
Halima Ali Mohamed kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) alisema makundi hayo matatu yanaonekana kuathirika zaidi na ukimwi, ambapo tafiti zinaonesha maambukizi yamefikia asilimia 30.
Aidha alisema kuna maambukizi yanayofikia asilimia 2.8 kwa wanafunzi wa vyuo vya mafunzo.
Tayari tafiti zinafanywaa kupata idadi kamili ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja (mashoga) pamoja na maeneo walipo ili iwe rahisi kuwafikia wakati wa utekelezaji wa mkakati huo.
Mkakati wa kwanza ulikuwa hauyakaribishi baaadhi ya makundi yakiwemo hayo kupata huduma kutokana na silka na utamaduni wa Zanzibar.
Alisema mkakati unalenga kupunguza kiwango cha taifa cha maambukizi kwa asilimia 33 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 0.6 hadi asilimia 0.4 ifikapo mwaka 2016.
“Lengo kuu ni kuzuia usambaaji VVU kwa Wazanzibari yakiwemo makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa ,kuwapatia huduma bora na kamili wanaoishi na VVU pamoja na kukabiliana na athari mbaya za kijamii zinazotokana na ukimwi,” alisema katika semina iliyowahusisha wadau mbali mbali wa masuala ya ukimwi.
Mapema Said Juma kutoka ZAC alisema mkakati wa kwanza uliomalizika mwaka 2009 kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa kutoa uelewa kuhusu masuala ya ukimwi lakini uelewa huo hauwiani na mabadiliko ya tabia kwa wananchi.
Katika upande wa huduma , MPIKU II unalenga kupunguza madhara ya kiafya na watu wanaoshi na VVU kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2016.
Aidha asilimia 80 ya wanaoishi na VVU watapata huduma za matibabuya magonjwa nyemelezi.
Wakichangia rasimu ya mkakati huo, washiriki wa semina hiyo walisema, vita dhidi ya ukimwi vinapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee hasa katika taasisi za elimu ya juu, ambapo baadhi ya washiriki walisema kuna udhalilishaji mkubwa dhidi ya wanafunzi wa kike unaofanywa na wahadhiri, ambao unaweza kuwa sababu ya kuongezeka maambukizi mapya ya VVU.
Aidha walisema tabia ya wanaume kuwa wanawake wengi (MCP) inahatarisha kuongezeka kwa maambukizi ya VVU na hivyo wakaishauri ZAC pamoja na taasisi nyengine zenye wajibu wa kutekeleza mkakati huo kutojikita zaidi katika makundi matatu na kusahau makundi mengine ambayo bado yako salama au maambukizi sio makubwa.
MPIKU II ambao utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2011/2016 utahakikisha kila taasisi za umma na asasi za kiraia pamoja na jamii wanashiriki katika mapambano dhidi ya Ukimwi ipasavyo.

No comments:

Post a Comment