Sunday 17 July 2011

ATOLEWA DONGE LA DAMU KILO 5.5 TUMBONI.

Atolewa donge la damu kilo 5.5 tumboni

Na Lulua Salum, Pemba
WANANCHI wametakiwa kubadilika na kuachana na imani potofu za kishirikina zaidi katika kutafuta tiba na badala yake wajenge tabia ya kwenda hospitali wanapojibaini na matatizo ya kiafya.
Kauli hiyo imetolewa na Ramon Contrera, daktari bingwa wa Upasuaji kutoka Cuba, ambae anafanyakazi katika hospitali ya Chake Chake Pemba, baada ya kukamilisha upasuaji mgonjwa alielazwa hospitalini hapo akisumbuliwa na tatizo la mayoma kwa muda mrefu.
Mgonjwa huyo alibainika kuwa na pande la nyama ndani ya tumbo lake lenye uzito wa kilogramu 5.5 ambalo amedumu nalo kwa muda mrefu na hiyo inadaiwa imechangiwa na hofu ya kwenda hospitali kutokana na umuhimu wa kukimbilia hospitali mapema badala ya kuelemea kwenye tiba za asili.
Daktari Ramon, alisema kujengeka kwa imani za kishirikina ndani ya nyoyo za watu wengi ni sababu ya ongezeko kubwa la maradhi na kupoteza maisha.
Alisema imefika wakati jamii kubadilika na kujenga tabia ya kuchunguza afya zao hata mwaka mara moja ili kujimbua endapo muhusika atakuwa amekumbwa na maradhi yoyote,
Daktari huyo bingwa ameishauri serikali iiangalie hospitali ya Chake chake na kuomba Serikali kuiangalia hospitali ya Chake Chake kwa kusema kuwa hospitali hiyo inafanya kazi nzito zisizolingana na ukubwa wa hospitali yenyewe,
Mgonjwa aliefanyiwa upasuaji huo ambae hakutaka kutaja jina lake gazetini alisema alisumbuka na tatizo hilo kwa muda mrefu na kuamini kwamba linaweza kuondoka kwa kufanya tiba za asili lakini aliona tatizo linazidi siku hadi siku na ndipo alipoamua kwenda hospitali kupatiwa tiba.
“Kiukweli nilishakata tamaa kabisa ya kupona tatizo hili lakini namshukuru Mungu kwani nimeshindwa kuamini kile kilichotoka tumboni mwangu ambapo awali niliamini nasumbuliwa na matatizo ya kiswahili,” alisema.

No comments:

Post a Comment