UN kuipatia Zanzibar bilioni 17.7
Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetiliana saini na Umoja wa Mataifa nchini Tanzania mpango wa msaada wa maendeleo wa shilingi bilioni 17.7 (dola milioni 11.6) unaanza mwezi huu hadi Juni mwaka 2015.
Hafla ya utiaji saini huo imefanyika jana, ukumbi wa Jumba la Makumbusho ya Kasri, Forodhani mjini hapa, ambapo kwa upande wa SMZ imewakilishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Khamis Mussa Omar na UN imewakilishwa na Mwakilishi Mkaazi wake Tanzania, Alberic Kacou.
Akizungumza mara ya utiaji saini hiyo, Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa,Tanzania, Alberic Kacou alisema mpango wa msaada huo umejumuisha mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Tanzania kwa ajili ya kutoa kipaumbele katika kukuza uchumi, huduma za afya ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI, lishe bora, elimu, mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, maji, utawala bora na msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi.
Alisema Mpango huo utatoa nafasi katika masuala ya uwajibikaji wa UN katika mchango wake kupunguza umasikini ikiwemo mikakati ya kitaifa ya MKUKUTA kwa Tanzania Bara na MKUZA II kwa Zanzibar ambao utanufaisha kwa ujumla, ambapo mwezi uliopita Juni 24 mwaka huu walitilia saini na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania jijini Dar es Salaam katika kutelekeza miradi mbali mbali, ambapo programu hiyo ya miaka minne itatumia Dola za Marekani milioni 777 kwa nchi mzima.
Alieleza mpango huo utasaidia Zanzibar katika kuimarisha uchumi kupitia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II), kujengea uwezo taasisi na kuongeza uzalishaji katika kilimo pamoja na huduma za kijamii hususani katika upatikanaji wa haki za binadamu katika viwango vya kimataifa.
Aidha alipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi, ambapo msaada huo utaongeza kasi za ukuaji wa uchumi.
Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Khamis Mussa alisema Zanzibar ina mashirikiano na muda mrefu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa katika kusaidia miradi mbali mbali ya kimaendeleo na kukuza uchumi, ikiwemo afya, elimu na kusaidia mpango mkuu wa miaka mitano Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).
Alieleza UN imeipatia Zanzibar shilingi bilioni 17.7 katika mpango huo wa msaada, ambapo kipaumbele ni sekta ya afya, elimu, mazingira katika kasi ya kukuza uchumi wa nchi.
Sunday, 17 July 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment