Atekwa nyara kwa kutaka kuuza mchele bei nafuu
• SMZ yawakoromea wafanyabiashara wanyanyasaji
• Yahamasisha wote wenye uwezo kuagiza bidhaa
Na Abdi Shamnah, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wafanyabiashara wenye uwezo wa kuleta bidhaa mbali mbali nchini, kufanya hivyo na kusema Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano.
Maalim Seif, ambae pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amesema hayo jana kwa nyakati tofauti alipozungumza na wananchi wa majimbo ya Matemwe na Chaani, kufuatia ziara zake za kuyatembelea Majimbo yote Unguja na Pemba kuonana na wajumbe wa CUF pamoja na kuzungumza na wananchi.
Amesema wakati huu wananchi wakilalamika kupanda kwa gharama za maisha kutokana na ongezeko la bei za bidhaa, kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaopinga hatua ya wafanyabiashara wengine kuleta bidhaa ikiwemo mchele kwa hofu ya bidhaa hizo kuteremka bei.
Alisema katika tukio la hivi karibuni kuna mfanyabiashara (hakumtaja jina) aliedhamiria kuleta mchele na kuuza kwa bei ya chini, lakini wamejitokeza baadhi ya wafanyabiashara wanaomtishia maisha kupitia meseji za simu, ili aondokane na dhamira hizo.
Bila kufafanua kwa undani, Maalim Seif alisema taarifa zilizopo ni kuwa mfanyabaishara huyo ametekwa nyara.
Alisema wafanyabiashara hao wanafanya hivyo kwa kuamini kuwa pale mfanyabiashara huyo atakapoleta bidhaa hizo na kuuza kwa bei nafuu, watalazimika kupunguza bei za bidhaa zao au zitawaozea madukani.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana na wafanyabiashara wote wenye dhamira ya kuwaondolea wananchi dhiki ya maisha inayotokana na kupanda kwa gharama za bidhaa pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo visivyokubalika na jamii.
Maalim Seif aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imedhamiria kunyanyua kipato chao kupitia mazao ya biashara, ikiwemo mwani ambao hivi sasa umekuwa ukiuzwa kwa bei ya chini mno.
Alisema Serikali imeipa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko jukumu la kuhakikisha bei ya zao hilo inapanda kama ilivyo kwa karafuu, na kubainisha changamoto iliyopo, kufuatia zao kutokuwa mikononi mwa Serikali.
Alisema hali ya bei ya zao hilo hivi sasa hairidhishi, kwani wakulima hulipwa wastani wa shilingi 400/- tu kwa kilo, wakati bei katika soko la dunia ni zaidi ya shilingi 2,500/-.
Aliwatupia lawama wafanyabiashara (matajiri) wanaojishughulisha na ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima, kwa kuwakandamiza kwa makusudi wakulima na kutoa visingizio vya uongo vya kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Alisema tayari kuna taarifa zinazoonesha nia ya kuja kwa makampuni yenye lengo la kupandisha bei ya zao hilo na hivyo kutoa ushindani katika soko la ndani ya zao hilo.
Aliweka wazi kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha bei ya zao hilo inapanda kutoka shilingi 400/- hadi kufikia shilingi 1,000/- kwa kilo, hatua aliyosema itamuwezesha mkulima kunufaika kutokana na jasho lake.
Katika hatua nyengine Maalim Seif aliwahakikishia wananchi wa Majimbo hayo kuwa Serikali imekusudia kulivalia njuga na kulizamaliza kabisa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama, ndani ya kipindi cha miaka mitatu, kupitia bajeti yake ya kila mwaka.
Vile vile Maalim Seif alitumia fursa ya kukutana na wananchi hao kuwaeleza azma za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bungeni mswada wa kuundwa kwa katiba mpya, hivyo aliwataka kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao bila woga, pale Tume itakapopita kukusanya maoni.
Aliwataka wananchi hao kutoa mawazo yao juu ya aina gani ya Muungano wanaoutaka na mambo mbali mbali yaliyomo ndani ya Muungano huo, ili hatimae Tanzania iweze kuwa na Katiba nzuri yenye maslahi kwa pande zote mbili za Muungano huo.
Monday, 25 July 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment