Thursday, 14 July 2011

UWT WATAKIWA KUCHAGUA VIONGOZI MAKINI.


UWT watakiwa kuchagua viongozi makini
Na Mwanajuma Abdi
WANAWAKE wa CCM wametakiwa wazidishe ushirikiano na upendo katika kuwachagua viongozi wenye uchungu wa nchi, wataoweza kukitetea  Chama hicho ili kiweze kuendelea kuwepo madarakani.
Rai hiyo imetolewa jana n mfanyabiashara, Mohamed Raza, katika hafla ya ujenzi wa taifa wa jengo la Umoja wa Wanawake Tanzania, Zanzibar (UWT), huko Mahonda, wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja.
Raza alimkabidhi Mwenyekiti wa UWT wa wilaya hiyo, Mwantakaje Nuru saruji mifuko 10, mabati 40 na misurumari yake, vikiwa na thamani ya jumla ya shilingi 960,000 ikiwa ni mchango wake katika jengo hilo lililofikia hatua za mwisho kumalizika.
Alisema bila ya mshikamano, akinamama, ambao wana ushawishi mkubwa kwa akinababa hakutoweza kupatikana viongozi wenye uchungu wa nchi na kukitetea Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwaondoshea umasikini wananchi, ikizingatiwa mwakani kuna uchaguzi wa ndani wa Chama hicho.
Alieleza kwamba wanawake wana mchango mkubwa katika kuimarisha Chama hicho na kukuza maendeleo ya kiuchumi kwa Zanzibar, hususan wakijikusanya pamoja katika vikundi vya ushirika na kuibua miradi mbali mbali.
Aliwahimiza waongeze mshikamano na  kukataa kuyumbishwa na kushawishiwa na watu wanaopenda uchu wa madaraka kwa maslahi yao binafsi.
Mfanyabiashara huyo, aliwaeleza akinamama hao kwamba wasikubali kutumiwa wala kugawiwa makundi na baadhi ya watu wanaotaka uongozi kwani watu wa namna hiyo hawana mustakabali mwema wa nchi.
Alifahamisha kuwa, ilani ya uchaguzi ya CCM imeweka wazi katika kuendeleza maendeleo, ambapo mchango alioukabidhi ni hatua hiyo ya utekelezaji ili kukifanya chama hicho kiwe imara. 
Aidha aliwaomba kinamama wa Mkoa wa Kaskani kuitumia Julai 31 mwaka, kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhani waandae mkutano maalum wa siku moja kueleza mafanikio na matunda ya Chama cha Afro Shirazi na kuahidi atagharamia maandalizi ya mkutano huo.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Salama Aboud, alimpongeza Raza kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia CCM, ambapo aliahidi kuendelea kumpa ushirikiano ndani ya Chama hicho.
Salama Aboud aliwaahidi akinamama hao kuwapatia korja 10 za miti kwa ajili ya kuezekea jengo lao ambapo Mwakilishi wa Jimbo la Amani Fatma Mbarouk alichangia shilingi 100,000 kwa ajili ya ujenzi huo.
Akisoma risala yao, Katibu wa UWT, wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja Narie Mbaraka alisema ujenzi huo umeanza Machi mosi mwaka jana, ambapo umejumuisha michango kutoka kwa viongozi mbali mbali wa CCM na Serikali na umeshagharimu shilingi milioni 2.6 na upo katika hatua za mwisho za kumalizika.

No comments:

Post a Comment