Friday, 15 July 2011

BILIONI 67 KUIJENGEA UWEZO ZAWA.

Bilioni 67 kuijengea uwezo ZAWA

Na Halima Abdalla
WIZARA ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, jana imetiliana saini na Kampuni ya Niras kutoka Denmark mradi wa kuijengea uwezo Mamlaka ya Maji (ZAWA) ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Hafla hiyo ilifanyika ukumbi wa jengo la Wizara hiyo Shangani mjini Zanzibar, ambapo kwa upande wa Zanzibar ilitiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Dk.Mustapha Ali Garu na Kampuni ya Niras ilisainiwa na mwakilishi wao Michael Juel.
Mradi huo utatumia zaidi ya shilingi bilioni 67 hadi kukamilika kwake na unatarajia kufaidisha zaidi ya watu 489,400 kwa kupatiwa huduma ya maji na usafi wa maskulini.
Akizungumza na watendaji kutoka Wizara ya Ardhi pamoja na wataalamu kutoka Kampuni ya Niras, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mwalimu Ali Mwalimu, alisema mradi huo wa miezi 24 utaanza mwezi ujao.
Alisema mradi katika kipindi hicho utaweza kuisaidia Mamlaka ya Maji kwa kuwapa elimu ya kuweza kuwajengea uwezo kuweza kufanya kazi kwa ufanisi, kusambaza maji na kupeleka katika vijiji tisa vya Unguja na Pemba.
Aidha alisema mradi huo pia utaweza kusaidia uimarishaji wa rasilimali maji nchini na sehemu ya vianzio vya maji.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Niras, Michael Juel, alisema kampuni yake ina uwezo wa kutosha kuhakikisha yaliomo katika mkataba yanatekelezwa.
Aidha aliahidi kufanya kazi kama inavyotakiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Dk. Garu kwa upande wake alisema ZAWA imefuata njia zote katika kuichagua kampuni ya Niras hivyo wana imani kampuni hiyo itatekeleza mradi huo kwa kiwango kinachokubaliwa.
Mradi huo ni seheu ya Mradi mkubwa wa maji unaoendeshwa Zanzibar kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ADB na UN-HABITAT.

No comments:

Post a Comment