Tuesday, 18 May 2010

Kumi waburuzwa mahakamani kwa tuhuma za unyangaji wa kutumia nguvu

VIJANA kumi wakaazi wa maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Magharibi Unguja, wakiwemo wanne wenye umri kati ya miaka 15 na 16, wamefikishwa Mahakamani Vuga, wakikabiliwa na tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu.
 
Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu, Nassor Ali Salim wa Mahakama ya Mkoa Vuga, na kusomewa mashitaka na Mwanasheria wa serikali, Sabra Mselem kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
 
Habari zilizopatikana kutoka mahakama hiyo jana, zinasema bada kukana tuhuma hizo, pamoja na upande wa mashitaka kutopinga dhamana juu yao, Hakimu Nassor Ali Salim aliwanyima dhamana watuhumiwa hao na kuwapeleka rumande kwa muda wa siku tisa.

Watuhumiwa hao ni Said Khamis Juma (15), Mkaazi wa Magogoni, Dadi Khamis Talib (15), wa Makondeko, Khamis Hamadi Bakari (19), anayeishi Magogoni, Makame Jumanne wa Magogoni na Othman Khamis Othman (21) Mkaazi wa Mwanakwerekwe.
 
Watuhumiwa wengine katika kundi hilo ni Rashid Mohammed Simba (10) wa Magomeni, wilaya ya Magharibi, Said Salum Hamadi (15), Khamis Mngwali Juma (18), Mohammed Said Salum (17) na Kassim Hamadi Abdallah (16) ambao wote ni wakaazi wa Magogoni.

Mapema, wakiwa mbele ya kizimba cha mahakama hiyo, Mwendesha Mashitaka, Sabra Mselem aliwasomea watuhumiwa hao shitaka la unyang’anyi wa kutumia nguvu kinyume na kifungu cha 285 na 286 (1) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
 
Katika maelezo yake, Sabra Mselem aliiambia mahakama kwa kudai kuwa, vijana hao kwa pamoja bila ya halali na kwa makusudi, waliyang’anya mali inayokisiwa kuwa na thamani ya shilingi 255,000.
 
Sabra aliiambia mahakama iliojaa waskilizaji kuwa mali inayodaiwa kuibiwa ni mabegi matatu ya nguo, radio Kaseti moja pamoja na fedha taslimu shilingi 200,000 mali ya Yussuf Ali Hamadi.
 
Kabla ya unyang’anyi huo, mahakama hiyo ya Mkoa ilifahamishwa kuwa waLIMshambulia Yussuf Ali Hamadi na Omar Juma Omar kwa kuwapiga mawe miguuni na kifuani na hatimae kufanikiwa kuwa nyang’anya mali hiyo, shitaka ambalo walilikana.
 
Pamoja na kukana huko, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, na kuiomba mahakama hiyo kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa pamoja na kutolewa kwa hati za wito kwa mashahidi.
 
Hakimu Nassor Ali Salim, alikubaliana na hoja hizo na kuliahirisha shauri hilo hadi Mei 26 mwaka huu kwa kusikilizwa, na kuutaka upande huo wa mashitaka kuita mashahidi siku hiyo.
Na Khamis Amani

No comments:

Post a Comment