KATIBU Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk, Mohammed Saleh Jiddawi amesema Zanzibar imepiga hatua nzuri katika mapambano dhidi ya Malaria na juhudi zaidi zinaendelea kuhakikisha mkakati wa kumaliza maradhi hayo unafanikiwa.
Kauli hiyo aliitoa jana kwenye ukumbi wa Hoteli ya Chavda Shangani mjini hapa, wakati akifungua mkutano wa sita wa majadiliano ya hali ya Malaria pamoja na mkakati wa kumaliza Malaria Zanzibar.
Alisema jitihada za pamoja kati ya serikali, wananchi na washirika wa maendeleo zimewezesha kwa kiasi kikubwa Malaria kupungua.
Dk. Jidawi amewataka wananchi kutobweteka na mafanikio hayo, badala yake waendelee kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa pamoja na kukubali kupigiwa dawa kwenye nyumba zao kufika kwenye vituo vya afya kupatiwa tiba sahihi ya Malaria mara watakapoona dalili za ugonjwa huo.
Nae Mratibu wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria PMI, Tim Ziemer, alisema Serikali ya Marekani kupitia mfuko wa Rais utaendeleza jitihada zake za kuipatia fedha Zanzibar katika mapambano dhidi ya Malaria ili kufikia lengo la kumaliza ugonjwa huo.
Alisema kwa sasa Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa ya mapambano dhidi ya Malaria na kinachohitajika ni kuongeza nguvu za kitaalamu na utoaji wa elimu kwa wananchi ili maradhi hayo yaondoke kabisa nchini.
Aidha amevitaka vyombo vya habari kusaidia katika utoaji wa elimu juu ya mapombano hayo.
Katika mkutano huo, mada mbali mbali zilijadiliwa ikiwemo sualala kuwabakisha watu tabia yaani BCC, ushughulikiaji wa mwenendo wa Maradhi, masuala ya upigaji dawa pamoja na matumizi ya vyandarua.
No comments:
Post a Comment