Tuesday 25 May 2010

Bodi rufaa ya kodi kusimamia malalamiko ya wafanyabiashara

Na Mwanajuma Abdi
BODI ya Rufaa ya Kodi Zanzibar, imesema itasimamia ipasavyo shauri la kodi litalofikishwa na walalamikaji wakiwemo watu wa kawaida, wafanyabiashara na Serikali katika upandishwaji na ulipaji kodi katika kipindi cha wiki moja ili haki itendeke.

Hayo aliyasema jana, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Khamis Ramadhan wakati akizungumza na waandishi wa habari huko, Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar.
 
Bodi hiyo itakuwa ikifanya kazi ya kupokea malalamiko hayo kwa muda katika Afisi ya Kitengo cha utawala na Huduma katika Wizara ya Fedha, hadi Afisi yao itakapokamilika katika jengo la zamani la Maktaba Kuu ya Zanzibar, Vuga mjini hapa.

Alisema Bodi hiyo itakuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa baina Bodi ya Mapato (ZRB) na Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato Tanzania (TRA), ambapo ndio wakusanyaji wa kodi mbali mbali kuanzia mshahara wa mfanyakazi, wafanyabiashara hadi wawekezaji waliopo nchini.
 
Alisema Bodi hiyo itakuwa ikisikiliza malalamiko ya wateja mbali mbali, watakaonesha vielelezo wanayoyalalamikia ili haki itendeke.
 
“Malalamiko hay pia yapo kwa Serikali kutokana na baadhi ya wawekezaji na wafanyabiashara kukwepo kulipa kodi kwa wakati, ambapo kuwepo kwa Bodi hiyo kutasaidia upatikanaji wa kodi ya SMZ katika kukuza maendeleo ya uchumi wa nchi,” Alifafanua
 
Mwenyekiti huyo, alifahamisha kuwa, Bodi hiyo inafanya kazi chini ya sheria namba moja ya mwaka 2006 na kanuni ya Aprili 21 ya mwaka huu, ilitangazwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar kupitia gazeti la Serikali ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila ya kuingiliwa na chombo chochote.
 
Alisema uamuzi wa kuwepo Bodi ya Rufaa ya Kodi Zanzibar umekluja kufuatia malalamiko mengi ya wafanyabiashara kutozwa kodi kubwa na ZRB na TRA, pamoja na Serikali kutolipwa mapato yake kwa wakati, huku serikali ikiwadai fedha nyingi wawekezaji na wafanyabiashara wanaochelewesha malipo ya kodi.

No comments:

Post a Comment