Saturday, 8 May 2010

Mvua zateketeza mashamba ya mpunga Zanzibar

• Wakulima roho juu wahofia kukosa mavuno
Na Haji Nassor, ZJMMC
WAKULIMA wa kilimo cha mpunga wanaolima kwenye maeneo yanayopitiwa na maji katika maeneo mbali mbali wilaya ya Magharibi Unguja, wamebainisha kuwa huenda msimu huu wasipate mavuno mazuri kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kusomba mipunga yao.

Walisema kuwa hali hiyo kwa sasa imekua ikiwaweka roho juu kwa vile baadhi ya shamba zao mipunga inakaribia kuchanua huku iking’olewa kutokana na nguvu za maji ya mvua.

Wakizungumza na mwandishi wa habari katika bonde la Melinane, shehia ya Kihinani,Chuini, Mbuzini na Bububu, wamesema kuwa mashamba mengi ya mpuga umeng’olea na maji.
 
Walieleza kuwa pamoja na kutumia nguvu nyingi kwa ajili ya kutayarisha kilimo hicho na kuwa na matarajio mema kwenye mavuno, wameshavunjika moyo na wanachoangalia kwa sasa ni rehema za Mwenyezi Mungu.
 
Mmoja kati ya wakulima hao Hassan Ali Mjaka (55) wa Chuwini, alieleza kuwa hapo awali,walikua wakilia kutokana na kilimo chao kukosa maji (mvua), lakini kutokana na kuchezwa na miongo wameshakumbwa na wasiwasi mkubwa juu ya kupata mavuno bora.

“Mwanzoni mwa matayarisho ya kilimo chetu hichi cha mpunga tulikua tukililia kwamba mara hii mpunga wetu hauna maji, na ndio maana baadhi yetu hata tulichelewa kusia (kumwaga mpunga), lakini sasa maji mengi na athari tumepata.
 
Nae Juma Mcha Juma ambae ni mkulima njia mbili (Mbuzini), alisema katika eneo lao pana mfano wa ziwa, na maji hutuwa kwa kipindi kirefu, ndio hasa wamepatwa na wasiwasi ya kutokua na mavuno ya uhakika.
 
Aliongeza kwa kusema kuwa, ufumbuzi pekee juu ya hilo kwa msimu jao ni kuhakikisha wanawezeshwa ili kupigia misingi shamba zao ili maji yanapokuja waweze kuyatumia kwa mujibu ya mahitaji yao.

Kwa pande wake Mwanajuma Mzombe Issa (50) wa Shehia ya Kikangoni, alisisitiza suala pekee la kuyakinga maji ya mvua ambayo hawayahitaji kwa matumizi ya papo hapo, ni kuwepo kwa misingi ya kudumu pembezoni mwa shamba zao ili kudhibiti hali hiyo.
 
Taarifa ambazo Gazeti hili imezipata zinaeleza kuwa zaidi ekari 40 za mpunga hususani zilizopo karibu na maeneo ya njia kuu za maji ya mvua katika maeneo mbali ya Kisiwani cha Unguja zimeharibika, hali ambayo inaashiria kutokuwepo kwa mavuno ya uhakika kwa baadhi ya maeneo.

No comments:

Post a Comment