Tuesday 18 May 2010

SACCOS ya elimu yajiandaa kutoa mikopo, kufanyakazi kama Benki

USHIRIKA Wa Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (Elimu Saccos) unakusudiwa kuimarishwa kwa kufanyiwa mabadiliko ili uweze kutoa mikopo kama zifanyazo benki mbali mbali hapa nchini.
 
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa ushirika huo Salma Simai Rajab mbele ya waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki, imeeleza kuwa mikakati ya kufikia hatua hiyo inatarajiwa kukamilika karibuni na kwamba lengo hilo likifikiwa, benki hiyo itakuwa na fursa nyingi za utoaji mikopo kwa wanachama na watu wengine.
 
Alisema kuwa hatua hiyo inafuatia ushirika huo ulioanzishwa mwaka 1997 kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi wafanyakazi wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kuimarika kifedha.
 
''Ushirika wetu umeimarika sana tulianza kutoa mikopo ya vifaa mbali mbali vikiwemo vya ujenzi na sasa tunakusudia kuufanya benki ili kutoa mikopo ya fedha, '' alisema Salma.

Alisema maandalizi ya kuubadili ushirika huo kuwa kuwa benki yameshaanza ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo yanayohusisna na masuala ya fedha baadhi ya wanachama wake ambayo yametolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB na Benki ya Maendeleo Vijijini CRDB.
 
Salma alifahamisha kuwa Benki zimekubali kuwa wafadhili wa ushirika huo kwa kutoa mikopo ya fedha ambazo hutumika kuwakopesha wanachama wa ushirika huo ambapo hivi karibuni benki ya CRDB iliupatia mkopo wa shilingi milioni 530 ushirika huo.
 
Alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika yenye Makao yake Makuu mjini Tunis Tunisia na ya CRDB ya mjini Dar es salaam zimeahidi kutoa mtaji wa fedha baada ya mipango ya kuanzisha BenkI hiyo kufanikiwa.

''Matumaini yetu ni kwamba tutafanikiwa kuugeuza ushirika wetu kuwa Benki hasa ukizingatia mshikamano tulionao kati ya Benki hizo zenye umaarufu na uwezo mkubwa,'' alisema Salma.
Na Issa Mohammed

No comments:

Post a Comment