IMESISITIZWA kuwa, suala la kujisajili kwa waajiri na waajiriwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) si la hiyari bali ni lazima kwa lengo la kustawisha hali za wafanyakazi nchini.
Hayo yamesemwa na Mwanasheria wa Mfuko huo Ramadhan Juma Suleiman alipokuwa akitoa mada katika mkutano kati ya uogozi wa ZSSF na waajiri kutoka taasisi mbalimbali nchini uliofanyika kwenye ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani juzi.
Mwanasheria huyo alisema kila mwajiri anapaswa kujisajili ndani ya siku 14 kutoka siku aliyoanza kuendesha mradi wake, pamoja na kuwasajili waajiriwa kwa kipindi kama hicho kuanzia siku ya uajiri wao.
Suleiman alieleza kuwa kushindwa kufanya hivyo, ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha mwaka mmoja jela au zote mbili kwa pamoja.
Kuhusu uwasilishaji michango katika ofisi za ZSSF, mwanasheria huyo alisema kwa mujibu wa sheria, mwajiri anawajibika kupeleka asilimia tano ya mshahara wa mwajiriwa na kuunganisha na mchango wake wa asilimia 10 ndani ya siku 14 pia.
Alifahamisha kuwa iwapo mwajiri atakwepa kutimiza wajibu wake, atahesabika amefanya kosa na hivyo atalazimika kulipa kiasi kama hicho pamoja na adhabu.
Makosa mengine ambayo alisema yanaweza kufanywa na mwajiri ni kukata asilimia tano ya mfanyakazi lakini akashindwa kuiwasilisha katika mfuko, pamoja na kukata au kuchukua chini ya kiwango kinachostahili kisheia.
Alisema kila mwajiriwa ambaye ni mwanachama wa ZSSF anayo haki ya kufuatilia katika ofisi za mfuko zilizoko Kilimani mjini Zanzibar ili kuhakikisha kama mwajiri wake anatimiza wajibu wa kuwasilisha michango hiyo.
“Kwa kuwa serikali imeridhia kuanzishwa kwa mfuko huu kwa nia njema kama zilivyo nchi nyengine, ni wajibu wa waajiri kufuata sheria ili kusaidia jitihada za kuwajengea wafanyakazi wetu mazingira mazuri ya kuishi pale muda wao wa kustaafu unapofika”, alifahamisha mwanasheria huyo.
Alisema pamoja na kufahamu ulazima wa kuchangia mfuko huo, baadhi ya waajiri wamekuwa wagumu kutekeleza wajibu wao, jambo linalolazimisha kuwepo na misuguano katika kuwafanya wafuate sheria ikiwa pamoja na kufikishana mahakamani.
Mapema akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Abdulwakil Haji Hafidh alisema, hifadhi ya jamii inalenga kuendeleza kipato cha mtu pale ajira yake inapokoma kwa sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu, ugonjwa, ajali, uzee pamoja na kifo.
Alisema ni haki ya msingi kwa kila mwananchi kuwa na hifadhi itakayomuhakikishia maisha mazuri anapokuwa nje ya ajira au kuwafaa warithi wake wakati maisha yake yatakapofikia hatima.
Hata hivyo alieleza kuwa imeonekana iko haja kuifanyia marekebisho sheria namba mbili iliyoanzisha mfuko huo ya mwaka 1998 ambayo ilifanyiwa mapitio makubwa na kuundwa upya mwaka 2005.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya mapitio ya matumizi ya hifadhi ya jamii na bajeti iliyotokana na mradi wa ILO-DFID, imeazimiwa kuleta mageuzi ya dhati kwa sekta ya hifadhi kwa kupanua wigo wake.
Hafidh alifahamisha kuwa miongoni mwa mapendekezo ya ripoti hiyo ni pamoja na kuufanya mfumo wa hifadhi ya jamii uwe wa wote ikizingatiwa kuwa wigo wa sekta hiyo ni mdogo ambapo hapa Zanzibar ni asilimia 6.6 tu ya watu wake ndio wenye hifadhi ya jamii.
Kutokana na tafiti kuonesha changamoto nyingi zinazoukabili mfumo wa hifadhi, alisema Bodi ya Wadhamini imeona iko haja ya kupata maoni na ushauri wa wanachama na wadau wengine ili kuufanyia marekebisho yatakayokidhi haja kulingana na mahitaji ya wakati uliopo.
Wanachama waliohudhuria mkutano huo walitoa mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuleta ufanisi kwa mfuko huo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa jumla.
Walitaka baadhi ya mambo ambayo yameonekana kuwa yanaleta urasimu yafutwe au kufanyiwa muundo mpya utakaowanufaisha waajiri na waajirwa kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment