Tuesday 25 May 2010

Wataalamu bado wanahitajika uchimbaji mafuta Z’bar-Nahodha

Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha amesema watalaamu wanahitajika katika suala la uchimbaji wa mafuta na kusimamia athari za kimazingira katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

Nahodha aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, baada ya Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid kufunga semina ya sikuiliyozungumzia mafuta na gesi asilimia.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar ni kuhakikisha inakuwa na wataalamu watakaosaidia kuepusha uchafuuzi wa mazingira ya baharini na nchi kavu wakati zoezi la uchimbaji mafuta litakapoanza.

Alisema watalaamu wa Norway katika semina hiyo wameonesha njia kwa kutoa rai jinsi ya kuwapata wataalamu wa ndani na nje katika kusimamia suala hilo, kwa vile litakapoanza athari za kimazingira zinaweza kujitokeza katika maeneo mbali mbali yakiwemo ya bahari na ardhini.

Alisema katika kukabiliana na athari hizo, lazima ziandaliwe mbinu za kukabiliana nazo kwa vile waathirika wakubwa ni wananchi.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume amekuwa akichukua jitihada mbali mbali kuboresha uchumi wa Zanzibar na katika kufanya hivyo ameimarisha miundo mbinu, ikiwemo umeme, barabara,maji, elimu na kilimo cha umwagiliaji maji.

Nahodha alisema Serikali imekuwa ikipitisha sera mbali mbali katika kukuza uchumi ikiwemo ya Utalii, ambapo suala la mafuta linahitaji kuwepo sheria madhubuti zitakazosaidia kuleta kasi ya maendeleo nchini.

Nae Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma, alisema semina hiyo imewasaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa kwa undani juu ya uchimbaji wa mafuta.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi Mwalim Ali Mwalim alisema utawala bora katika uchimbaji wa mafuta unahitajika kuweza kufaidika nayo.

Alifafanua kuwa, mafuta kuwepo au kutokuwepo kunahitaji kufanyika kwa uchunguzi wa muda mrefu, ambapo baadhi ya nchi kama Zanzibar zimeanza kuona dalili za viashirio katika bahari na ardhini, ambapo Zanzibar nako kunaonesha dalili hizo.

Akifunga semina hiyo, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, amesema serikali itawasomesha vijana 10 nje ya nchi kuhusu njia za uchimbaji mafuta likiwemo la uangalizi wa athari za kimazingira.

Alisema Serikali itahakikisha kuwa, sheria ya mafuta na gesi asilia inakwenda sambamba na kuangalia sekta nyengine zikiwemo usalama wa fedha katika kukabiliana na rushwa.

Semina hiyo iliwashirisha Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria na Watendaji kutoka Taasisi mbali mbali za SMZ na wataalamu wa Norway ambao ni wakufunzi wa mafunzo hayo ya siku mbili.

No comments:

Post a Comment