Saturday, 1 May 2010

Mbwembe zatawala ‘May day’ Zanzibar

Na Maryam Ally (MSJ)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume jana aliyapokea maandamano ya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi katika viwanja vya Hoteli ya Bwawani mjini hapa.
 
Maandanamo hayo ni maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani, ambayo huadhimishwa kila ifikapo Mei Mosi ya kila mwaka.
 
Kauli mbiu ya mwaka huu, ‘Mei Mosi ni siku ya Wafanyakazi Duniani, Uchaguzi Usaidie Kuimarisha Maslahi na Ushirikishwaji wa Wafanyakazi’, ambapo ujumbe huo unakwenda sambamba na mwaka wa uchaguzi mkuu unaotegemea kufanyika Oktoba 31 nchi nzima.
 
Maandamano hayo yalianzia Malindi na kumalizikia katika Hoteli ya Bwawani, ambayo yaliongoza na Bendi ya Chipukizi, sambamba na kuwepo kwa Taarabu iliyokuwa ikitumbuiza katika viwanja vya Hoteli hiyo, sambamba na sherehe hizo kupambwa na utezi maalum kwa shughuli hiyo.
 
Rais Karume pia alipata nafasi ya kukabidhi zawadi ya fedha taslim na vyeti kwa wafanyakazi bora sita kwa niaba ya wenzao, ambao jumla yao ni 76, sambamba na kumkabidhi zawadi Waziri wa Kazi, Asha Abdallah Juma aliyotunukiwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa kuongoza vizuri Wizara hiyo na kusimamia maslahi ya wafanyakazi.

Katibu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohammed alisema wafanyakazi wanalalamikia kwa miaka miwili kukatwa fedha kwa ajili ya vitambulisho vya kazi, sambamba na wimbi la kuwepo kwa mishahara hewa kama wahusika wanachukuliwa hatua gani.
 
Aidha alieleza kilio chengine ni wadai ya wafanyakazi hususani wa sekta binafsi kupewa mikataba na waajiri wao, jambo ambalo linawasababishia kupata fursa na haki zao kama waajiriwa wengine.

Katibu huyo, alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni kuwasaidia wastaafu kuongezwa fedha katika pencheni zao ili ziweze kwenda sambamba na nyongeza za mishahara inapofanyiwa marekebisho kwa wafanyakazi waliokuwepo makazini.
 
Mwakilishi wa Chama cha Uajiri Zanzibar (ZANEMA), alihimiza kuwepo kwa mashirikiano baina ya wafanyakazi na waajiri ili kuongeza ufanisi wa kazi katika kuiletea maendeleo makubwa Zanzibar na kukuza uchumi wan chi.
 
Hata hivyo, alishauri juhudi makusudi zichukuliwe ili kuwajengea uwezo wafanyakazi na wananchi kwa ujumla ili waweze kuingia katika ushindani wa soko la ajira, likiwemo la soko la pamoja la Afrika Mashariki linalotegemea kuanza Julai mwaka huu kwa nchi zote wanachama.
 
Alieleza juhudi hizo pia zielekezwe kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kukuza elimu ya amali na kuongeza kwa vyuo vya amali vitavyowasaidia vijana kupata taaluma hiyo ili waweze kujiajiri na kuingia katika soko hilo.

No comments:

Post a Comment