Wednesday 5 May 2010

Rais Karume aridhishwa na mchango wa IFAD kwenye kilimo

Na Rajab Mkasaba, Dar es Salaam
MFUKO wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), umeeleza kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kusaidia mikakati ya kutafuta ufumbuzi wa kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo Zanzibar hasa nzi wa matunda.

Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Kanayo Nwanze, aliyasema hayo jana alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, katika Hoteli ya Moevenpick Royal Palm mjini Dar-es-Salaam.
 
Dk. Karume na na kiongozi huyo wa IFAD, walikutana baada ya kikao cha asubuhi cha mkutano mkuu wa kiuchumi duniani kuhusu bara la Afria (WEF), uliozungumzia juu ya suala la kilimo.
 
Nwanze alimueleza Rais Karume kuwa mfuko huo umefarajika na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wake katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo IFAD, itaendelea kuunga mkono juhudi hizo na kusisitiza kuwa miongoni mwa mipango iliyoweka katika kuimarisha sekta ya kilimo ni pamoja na kuendeleza mradi mkubwa wa kifedha utakaovinufaisha vikundi vya wanawake.
 
Nwanze leo atafanya ziara ya siku moja Zanzibar ikiwa ni pamoja na kutembelea vikundi vya kilimo, vikundi vya akinamama pamoja na kuangalia mradi wa kuua wadudu waharibifu wa kilimo huko Mwakaje.
 
Alieleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kazi hiyo nzuri iliyooneshwa na vikundi vya kilimo, Mfuko wake utasaidia kuongeza nguvu ili kuona kazi hiyo inapata mafanikio baada ya majaribio ili iweze kutumika kwa wakulima wa mazao ambayo yamekuwa yakisumbuliwa na wadudu kwa muda mrefu.
 
Rais huyo wa IFAD alieleza kuwa zaidi ya dola za Marekani milioni 150 zimetengwa na IFAD kwa kushirikiana na taasisi nyengine za kimataifa kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini Tanzania ambapo pia Zazibar itafaidika na fedha hizo.

Alisema kuwa tayari nchi mbali mbali zikiwemo za Asia, Amerika ya Kusini na Afrika zimo katika mchakato wa mradi huo mkubwa wa kuimarisha sekta ya kilimo uliochini ya IFAD.

Nae Rais Karume kwa upande wake alimueleza Kiongozi huyo kuwa amefarajika kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za Mfuko huo za kuimarisha kilimo Zanzibar.

Rais Karume alimueleza Nwanze kuwa hatua hiyo ya kuunga mkono vikundi vya akinamama vya kuimarisha kilimo Zanzibar ni jambo la busara kwa maendeleo ya wanawake na taifa kwa jumla.
 
Alieleza kuwa kumsaidia mwanamke ni hatua nzuri na jambo kubwa katika jamii na kusisitiza kuwa unapomuelimisha mwanamke mmoja na kumjengea uwezo ni sawa na kuielimisha jamii.
 
Alisema kuwa kutokana na Zanzibar kutegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii ni jambo la busara iwapo sekta ya kilimo itapewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika sekta ya utalii.

Rais Karume alieleza haja ya kuwajengea uwezo wakulima kwa kuwapa elimu itakayowasaidia katika kuimarisha sekta ya kilimo na kusisitiza kuwa sekta hiyo pia imekuwa ni mkombozi katika suala zima la ajira.

Rais Karume alimueleza kiongozi huyo hasara kubwa inayofanywa na wadudu hao na kumtaka kusaidia katika kupambana nao.
 
Aidha, Rais Karume alieleza kufarajika kwake na azma ya IFAD ya kuunga mkono na kuongeza nguvu kwa kikundi cha kijamii katika suala zima la utafiti juu ya kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo.
 
Katika mazungumzo yake Rais Karume alieleza kuwa umefika wakati wa kuweka mikakati madhubuti juu ya kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kutafuta njia juu ya maendeleo ya sekta hiyo.

Sambamba na hayo, Rais Karume alisema kuwa ipo haja katika kukuza sekta hiyo ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wakulima wadogo kwa kuwajengea uwezo wa kifedha pamoja na masoko na hivyo kutoa wito kwa mabenki kuekeza katika sekta hiyo.
 
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa IFAD Tanzania, Dk. Mwatima Juma alieleza kuwa mradi huo mkubwa pia utasaidia miundombinu ya kilimo, ukuzaji wa uwezo wa kifedha kwa vikundi vya kilimo pamoja na kuunga mkono mikakati megine ya kilimo Zanzibar.

Dk. Mwatima alieleza hatua za IFAD za kushirikiana na wananchi katika utafiti wa kutumia viungo kwa ajili ya kutengenezea dawa ya wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo wakiwemo inzi.

No comments:

Post a Comment