Saturday 8 May 2010

Zoezi la kuandikishwa waliokosa vitambulisho ladorora

Na Mwanajuma Abdi
ZEOZI la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, linaloendeshwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwa watu maalum walioorodheshwa baada ya kukosa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi katika zoezi lililopita, limeanza kwa kusuasua, huku idadi ndogo ya watu waliojitokeza.

Waandishi wa habari waliotembelea katika vituo vya Mkoa wa Mjini Magharibi, wamejionea idadi ndogo ya watu waliojitokeza kujiandikisha.

Zoezi hilo la siku mbili, ambalo limeanza jana, na leo litamaliza kwa wilaya zote 10 za Unguja na Pemba kwa watu maalum walioorodheshwa na Tume hiyo, Februari 22 hadi 28 mwaka huu, waliokosa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, wakati wa uandikishaji ulipofanyika wa awamu ya kwanza na wa pili Zanzibar mzima.
 
Gazeti hili lilipata nafasi ya kuzungumza na Afisa wa wilaya ya Magharibi Unguja, Suluhu Ali Rashid katika kituo kilichopo Skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’, alisema idadi ya watu waliojitokeza ni ndogo katika zoezi hilo maalum.
 
Alisema hadi kufikia majira ya saa 6.40 mchana watu waliojitokeza kujiandikisha ni 12 katika kituo hicho kati ya watu 337 walioorodheshwa katika daftari hilo.
 
Alieleza changamato nyengine zinawakabili katika hicho ni pamoja na kwenda watu wengi, ambao hawamo katika orodha ya majina waliyonayo kituoni hapo, wengi wanaojitokeza wakidai hawakuwepo nchini.
 
Aidha alifahamisha kuwa, watu hao waliwarejesha kwa vile zoezi hilo halihusiani na kesi zao, kwani zoezi la uandikishaji huo halihusishi masheha wala mawakala wa vyama hivyo sio rahisi kuwakubali watu waliokuwa hawamo katika orodha yao waliyoitayarisha.
 
Nae Afisa wa Uandikishaji wa wa wilaya ya Mjini, Khadija Ali, alisema zoezi linakwenda vizuri, ambapo hadi majira ya mchana watu 32 wameshaandikishwa kati ya watu 100.

Hivi juzi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ilitangaza kwamba zoezi hilo litaendeshwa jana (Mei 8 hadi 9 mwaka huu) kwa nchi nzima.
 
Aidha taarifa hiyo imefafanua kuwa watakaohusika ni wananchi walioorodheshwa majina yao katika zoezi lililofanyika Februari 22 hadi 28 mwaka huu, ambao tayari wameshapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, ndio wataohusika na zoezi hilo la siku mbili Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment