Saturday 8 May 2010

Kijana ajitokeza kumrithi Mbunge Laizer Arusha

MBUNGE wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Lekule Laizer ameendelea kupata wapinzani, baada ya Mkurugenzi wa shirika la wafugaji la Elimu na Afya (LOPEHCO), Kashuma Ole Sayalel kutangaza kugombea kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Jimbo hilo.
 
Sayalel amekuwa mwanachama wa CCM wa pili kutangaza kuwania kiti hicho, ambapo awali mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Arusha, Francis Ole Ikayo pia alitangaza kugombea kiti hicho ambacho, Laizer atakuwa akikitetea.
 
Akizungumza, Sayalel alisema ameamua kugombea ubunge ili kusaidia kuokoa maisha ya jamii ya wafugaji ambao wanaendelea kuwa masikini kutokana na kukosa utetezi wa haki zao na kupewa mbinu sahihi za kubadilisisha maisha yao.
 
"Hali ya wafugaji wa jamii ya kimasai Longido ni mbaya sana licha ya kuwa na rasilimali nyingi kama wanyamapori na madini, naimani ninaweza kushirikiana na wadau wengine kuboresha maisha ya wananchi wa Longido"alisema Sayalel.
 
Alisema hivi sasa vijana wengi wa kimasai wa Longido wamekimbilia mijini kufanyakazi za ulinzi kutokana na maisha duni ambayo yamechangiwa na ukame ambao mwaka jana uliua mifugo yao kwa kukosa malisho na kushindwa kupewa njia mbadala ya kuendesha maisha yao.
 
"Leo hii vijana wa Longido wamejaa mjini wanalinda, wasichana wanafanyabiashara za kuuza kuni na vitu vingine ambavyo havina tija kwao hivyo naamini nina uwezo wa kukaa na makundi haya ya vijana wenzangu na kupeana mbinu mpya za kubadilisha maisha yetu"alisema Sayalel.
 
Alisema wilaya ya Longido ni moja ya wilaya ambazo zina matatizo makubwa ya miundombinu, upatikanaji wa maji na mahitaji mengine muhimu hali ambayo imemsukuma kugombea ili ashirikiane na wadau wengine kupunguza kama sio kumaliza matatizo ya wilaya hiyo.

Wilaya ya Longido ambayo awali ilikuwa ni sehemu ya wilaya ya Monduli, imekuwa ikiongozwa na Mbunge wake, Lekule Laizer kwa zaidi vipindi viwili sasa.
Na Ramadhani Juma, Arusha

No comments:

Post a Comment