Saturday, 1 May 2010

Dk. Karume: Viongozi wasiojali maslahi ya wafanyakazi 'watoswe'

Ni katika uchaguzi mkuu 2010
• Wafanyakazi, wakulima ndiyo wakombozi wa Zanzibar
• Serikali kuendelea kujali maslahi ya wafanyakazi

Na Mwanajuma Abdi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amewaeleza wananchi kwamba viongozi wasiopenda maslahi ya wafanyakazi watoswe katika nchi na wala wasipewe nafasi ya kuwaongoza katika uchaguzi mkuu utaofanyika mwaka huu.

Dk. Karume aliyasema hayo jana, wakati akiwahutubia mamia ya wafanyakazi waliofurika katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar katika maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo husherehekea duniani kote kila ifikapo siku hiyo.
 
Alisema viongozi hao wapo, ambao wanapinga maslahi ya wafanyakazi na sio wana mapinduzi wa kweli kwani Mapinduzi ya 1964 ya Zanzibar yalifanywa na wafanyakazi na wakulima kwa lengo la kujikomboa na udhalili waliokuwa wakifanyiwa na wakoloni na sultani.
 
"Viongozi wasiopenda maslahi ya wafanyakazi sio wana Mapinduzi na mimi nawajua wapo kwani nchi hii ilipinduliwa na wafanyakazi na wakulima kwa lengo la kupata fursa ya kujitawala wenyewe na kupata haki zao", alifafanua Dk. Karume.

Kauli mbiu ya mwaka huu, 'Mei Mosi ni siku ya Wafanyakazi Duniani, Uchaguzi Usaidie Kuimarisha maslahi na Ushirikishwaji wa Wafanyakazi, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafahamu umuhimu wa wafanyakazi ambao ni mhimili mkubwa wa nchi tokea Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
 
Aliwataka wananchi kujiepusha na vurugu za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao, ambapo aliwasihi watofautiane kwa kupingana katika mawazo na sio kupigana, kwani siasa hizo zimepitwa na wakati.

Alisema uchaguzi ukifika kila mtu ana chama chake aende akapige kura halafu arudi kwake bila kusababisha vurugu zitazopelekea watu wapigane.
 
Aliongeza kusema kutokana na sababu hiyo Serikali imekuwa ikipokea na kufanyia kazi ushauri na fikra zinazotolewa na wafanyakazi kupitia vyombo mbali mbali vya kisheria, jambo ambalo limesaidia sekta ya kazi Zanzibar kukua na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

Alieleza maadhimisho hayo yametokana na maandamano ya wafanyakazi huko Chicago Marekani mwaka 1889 wakidai haki na maslahi bora kazini ili kutoa fursa kwao, kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
 
"Historia yake ina mengi lakini la msingi ni mshikamano wa wafanyakazi duniani na uhusiano wao na waajiri, kutokana na hayo, Jumuiya ya kimataifa ilianzisha chombo maalum cha kimataifa cha kushughulikia masuala ya kazi yaani Shirika la Kazi Duniani (ILO)", alisema.

Alieleza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ya awamu ya sita wakati ilipoingia madarakani mwaka 2000, imekuwa ikishughulikia masuala ya wafanyakazi ikiwemo mishahara, viinua mgongo na pencheni, ambapo katika kipindi cha Januari 2005 hadi Disemba 2009 wastaafu 8,609 wamelipwa mafao yao yenye thamani ya shilingi bilioni 26.26.
 
Rais Karume alisema kima cha chini cha mishahara kilipanda kutoka shilingi 25,000 mwaka 2000 hadi kufikia shilingi 100,000 mwaka huu.

Aidha aliongeza kusema katika kuwajali wafanyakazi Serikali imetumia shilingi bilioni 5.80 kulipia mishahara mwezi Oktoba 2009, kutoka shilingi bilioni 5.30 mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2009-2010 kufuatia awamu ya pili ya ongezeko la mishahara.
 
"Mnamo mwezi uliopita Serikali imetumia shilingi bilioni 6.72 kufuatilia malipo yaliyotokana na muundo mpya wa utumishi wa walimu, hatua hiyo inadhihirisha jinsi ambavyo Serikali inavyowakumbuka na kuwajali wafanyakazi wake kila hali inaporuhusu", alisisitiza Rais Karume.

Dk. Karume aliwaeleza wafanyakazi hao kwamba, wastaafu waliostaafu hivi karibuni hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu, tayari wameshafanyiwa mahesabu ya fedha zao na kulipwa viinua mgongo vyao wanavyostahiki, ambapo kwa wale waliostaafu mwezi wa Februari watalipwa viinua mgongo vyao kuanzia wiki ya mwanzo ya mwezi huu.
 
Rais Karume alisema, Serikali imesikia kilio cha siku nyingi kuhusiana na matatizo ya wafanyakazi katika sekta ya umma, ambapo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na washirika wengine wapo katika utaratibu wa kurekebisha mfumo wa sekta hiyo, ukiwemo wa uajiri, uwajibikaji pamoja na utaratibu bora wa kupandisha mishahara kwa wafanyakazi.
 
Aidha alifahamisha kuwa, katika sekta binafsi, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), unaangalia utaratibu bora zaidi wa upandishaji mishahara, ambapo Waziri wa Kazi, ameshadokeza kama mtaalamu elekezi ameshateuliwa kufanya utafiti wa mishahara hapa nchini.
 
Alisema ripoti ya utafiti huo utapatikana mapema mwezi Juni, 2010, na kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Akizungumzia mtikisiko wa uchumi duniani, alieleza mwaka juzi (2008), alisema nchi zilizoendelea ziliyumba kiuchumi na athari zake zilijitokeza katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, Zanzibar, kwa kupanda gharama za maisha kutokana kupanda kwa bei ya chakula na mafuta, jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa mfumuko wa bei.
 
Dk. Karume alisema mwaka juzi pia Zanzibar ilipata matatizo makubwa ya kuharibika kwa waya wa umeme kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar, uliosababisha ukosefu wa huduma hiyo kwa mwezi mmoja.
 
Sambamba na mwezi Disemba mwaka jana hadi Machi nchi imeshuhudia tukio jengine la kukatika kwa umeme kwa miezi mitatu mfululizo, mchanganyiko wa matatizo hayo nchi iliathirika kiuchumi katika maeneo ya utalii, biashara, pamoja na shughuli za viwanda.
 
Alieleza kwamba uchumi wa wananchi na maisha ya kawaida yaliathirika na mapato ya Serikali yalishuka, ambapo aliwapongeza wafanyakazi na wakulima kuwa pamoja na matatizo hayo hawakukata tamaa waliendelea kujenga mshikamano, kuimarisha umoja kati yao na kuongeza juhudi katika utendaji wa kazi, jambo ambalo wameisaidia kuiokoa nchi na janga.

Aliendelea kusema katika kuimarisha juhudi za miundombinu ya kiuchumi ikiwemo umeme wa uhakika, jana (juzi), walishuhudia tukio kubwa la utiaji saini mkataba wa utiaji wa laini mpya ya umeme wa megawati 100 kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar.
 
Alisema mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC), ambao utasaidia kuimarisha uwekezaji wa vitega uchumi Zanzibar na kusaidia ukuaji wa ajira na mapato kwa wananchi.
 
Rais Karume alifafanua kuwa, mwezi Novemba mwaka jana, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilitia saini mkataba wa soko la pamoja baada ya majadiliano ya muda mrefu, ambapo alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar, hususani vijana kutumia fursa zitakazokuwepo katika makubaliano hayo.
 
Alisema Wizara ya Kazi imeshafanya mpango wa kuwa na kitengo cha taarifa za kazi, ambapo aliagiza Wizara hiyo, kukamilisha hatua muhimu zilizobakia ili waweze kutoa taarifa zitakazowasaidia vijana na wananchi kufaidika na soko hilo.
 
Nae Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma, alisema wafanyakazi ni sehemu ya jamii bila ya kuwepo wao uajiri utakuwa hakuna na bila ya kuwepo kazi hakuna uhai.
 
Alieleza sera na kanuni zinaandaliwa ili ziwepo sheria zitazotoa fursa ya upandishaji wa mishahara ya kiima cha chini ili wafanyakazi waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Aidha alitoa wito kwa wawekezaji kuwaajiri wazalendo kwa kazi wanazoziweza na waache tabia ya kuwafukuza ovyo kazi, sambamba na kuwafungisha mikataba ya kazi kwa ajili ya kupata haki zao baada ya kumaliza muda wao wa kazi.
 
Mapema Makamo Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar, Suleiman Ali Omar, wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Rais Karume alimuambia zawadi waliyompatia ni kutokana na kufanya kazi vizuri katika kuwatumikia wananchi kwa muda wote.

No comments:

Post a Comment