Tuesday 4 May 2010

Masheha Kusini toweni ushirikiano kukabili uhalifu-Polisi

Na Fauzia Muhammed
MASHEHA wa katika Mkoa wa Kusini Unguja wametakiwa kutoa ushirikiano wa kuwabaini wageni wanaoingia katika shehia zao ili kuhakkisha masuala ya uhalifu yanapigwa vita.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa upelelezi ya makosa ya jinai Mkoa wa kusini Unguja Makarani Khamis alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Mwera.

Makarani alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza matukio ya uhalifu yanayongezeka kila kukicha kwenye shehia na mitaa mbali mbali.

Aidha, Makarani alifahamisha kuwa pamoja na ulinzi wa doria ulioanza kwenye vijiji mbali mbali, pia ipo haja kwa masheha kuwa waangalifu kuhusu wageni wanaoingia kwenye shehia zao ili kudhibiti uhalifu.
 
Makarani alizitaja sehemu hizo ambazo zimeshaanza kupata huduma ya ulinzi wa doria kuwa ni Hawaii na Mwera Mtofani.
 
Vile vile alieleza kuwa polisi wamejianda kufanya msako wa mara kwa mara, ndani ya mwezi mmoja ili kuhakikisha uhalifu unapungua ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
 
Hivyo, Makarani amewataka wananchi wema kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano katika sehem zinazo husika ili kuhakikisha uhalifu unapungua zaidi katika Mkoa huo.

No comments:

Post a Comment