Tuesday, 4 May 2010

Wapiga kura 67,789 waandikishwa awamu ya pili Pemba

ZOEZI la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili limemalizika katika wilaya zote nne kisiwani Pemba baada ya kufanyika kwa muda wa siku 63 kwa majimbo yote 21.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Msaidizi Afisa wa Uandikishaji Pemba, Ali Mohammed Dadi, alisema katika zoezi hilo jumla ya wapigakura wapatao 67,789 wameandikishwa .

Dadi alisema katika zoezi hilo wanawake wapatao37,002 na wanaume wapatao 30,787 walijitokeza katika shehia zao kwa kujiandikisha katika daftari hilo, jambo ambalo litawawezesha kutumia demokrasia yao wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
 
Akizitaja takwimu hizo kiwilaya afisa huyo alisema wilaya ya Wete jumla ya wapiga kura 27,080 wakiwemo wanawake 14,650 na wanaume 12,430 wakati katika wilaya ya Chake Chake, jumla ya wapiga kura 18,227, wakiwemo wanaume 8,177 na wanawake 10,050 walijiandikisha kwa awamu hiyo.
 
Wilaya ya Mkoani jumla ya wapiga kura 17,813 walijitokeza kujiandikisha katika zoezi hilo wakiwemo wanawake 9,768 na wanaume 8,045 na wilya ya Micheweni jumla ya wapiga kura wapatao 4,669 wakiwemo wanawake 2,534 na wanaume 2,135 walijiandikisha katika zoezi hilo la awamu ya pili.
 
Alieleza katika zoezi hilo lililoanza Machi 1 na kumalizika Me 2, akinamama wameonekana kujiandikisha kwa wingi kuliko wanaume na kufikia asilimia 54.6.
 
Dadi alisema pamoja na malalamiko ya hapa na pale lakini hakupata barua yoyote katika ofisi yake inayo lalamikia zoezi hilo la awamu ya pili.
 
Hivyo amewataka wale wote waliondikishwa katika daftari hilo, kutunza risiti zao jambo ambalo litawapa urahisi wakati wa kuchukua vitambulisho vyao.
Na Bakar Mussa, Pemba

No comments:

Post a Comment