Saturday 1 May 2010

Mashindano ya biashara kukuza pato la Taifa

WAZIRI wa Utalii, Biashara na Uwekezaji Zanzibar, Samia Suluhu Hassan, amesema mashindano ya biashara kwa vikundi yatasaidia kujenga utamaduni wa ushindani kwa wafanyabiashara wadogo wadogo katika kuongeza pato lao na Taifa kwa ujumla.
 
Hayo aliyasema, wakati akizindua mashindano ya biashara kwa vikundi, sambamba na ugawaji fomu za maombi kwa mashindano hayo, ambayo yanafadhiliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar (ZNCCIA) na Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Baharini na Ukanda wa Pwani (MACEMP) yaliyofanyika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Kauli mbiu ya mashindano hayo ni ‘Usichelewe, Mtaji ndio Huu, Kuza Mradi wako’, ambao una lengo la kuwashajiisha wafanyabiashara, wakulima, wavuvi kujiweka katika vikundi vya kufanya mkakati wa maendeleo ya miradi yao ili waweze kupata ushindi katika mashindano hayo.
 
Alisema mashindano hayo yatajenga utamaduni kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, wavuvi, wakulima na wazalishaji wa bidhaa mbali mbali katika kuongeza kasi katika kuimarisha miradi yao katika kukuza uchumi wa nchi na wao kujikomboa na umasikini.

Waziri Samia alipongeza ZNCCIA kwa kushirikiana na Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Baharini na Ukanda wa Pwani (MACEMP) kwa kuandaa mashindano hayo kwa kuwahusisha moja kwa moja wafanyabiashara wadogo wadogo na makundi ya wakulima na wavuvi wa Unguja na Pemba ili kuibuka na ushindi.

Alisema washindi watakaopatikana katika mashindano hayo wataweza kusaidiwa ruzuku, vitendea kazi na kujengewa uwezo wa kitaaluma kwa kujiimarisha katika shughuli zao na kuondokana na umasikini badala ya kupatiwa fedha kama huko nyuma, ambapo wengi wao walifeli kutokana na matumizi mabaya ya pesa hizo.
 
Alieleza fedha ni bilisi zinaweza kuwaletea tabu bila ya kujua, hivyo amewapongeza Jumuiya hiyo na Mradi wa MACEMP kwa kubuni njia nzuri ya kuwasaidia kwa vitendea kazi na kujengea uwezo wa kitaalamu kwa ajili ya kujiendeleza kwa ufanisi mkubwa na kuwaongezea mapato.

Samia alifahamisha kuwa, nchi nyingi duniani zimeweza kukuza uchumi wake kwa kuwajengea uwezo wafanyabiashara hususan wa chini, kwani wao ndio wanaoongeza pato kuu la Taifa kuliko wafanyabiashara wa daraja kubwa.

Alisema nchi kama Italia imeweza kufanya vizuri katika uchumi wake baada ya kuwawezesha wafanyabiashara wake wadogo wadogo na kuwanyanyua hadi kufikia wa kati, ambapo hivi sasa wamewekeza hadi Zanzibar katika miradi mbali mbali.

Aidha alieleza kufanyika kwa mashindano hayo ni hatua kubwa iliyofanywa na Jumuiya ya ZNCCIA na mradi wa MACEMP wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kushirikisha sekta za watu binafsi katika kuwanyanyua wananchi ili kuondokana na umasikini ifikapo mwaka 2020.
 
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Rais wa ZNCCIA, Abdallah Abass, alisema lengo la mashindano hayo ni kujenga ushindani miongoni mwa wafanyabiashara wa Zanzibar, ambapo mshindi atapatiwa nyenzo, taaluma, vifaa kwa ajili ya kuendeleza vikundi vyao katika miradi mbali mbali wanaojishughulisha nayo, sambamba na kunyanyua biashara.

Nae Kaimu Meneja wa Mradi wa MACEMP, Mohammed Sudi, alisema mradi huo ni wa miaka sita, ulianzia Disemba 2005 hadi 2011, ambapo hadi sasa umesaidia miradi 251 kati ya hiyo 114 Unguja na 137 Pemba na jumla ya shilingi milioni nne zimeshatumika kwa kuwasaidia wananchi katika miradi yao.

Aliongezea kusema mradi huo una lengo la kusimamia ukanda wa pwani katika suala zima la uchafuzi wa mazingira na kuwaongezea kipato cha wananchi katika kuwasaidia kuwapa nyenzo katika kuwaendeleza katika miradi yao ili kukuza uchumi wa nchi.
Mwanajuma Abdi na Maryam Ally, MSJ

No comments:

Post a Comment