Na Mwantanga Ame
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewataka wanachama wa CCM Jimbo la Kitope kuchagua viongozi wataoweza kuchagulika katika ngazi zote.
Hayo aliyasema jana katika sherehe fupi ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Jimbo hilo.
Katika ujenzi huo, alichangia kwa kutoa shilingi milioni 15 ambazo alimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Idd.
Waziri Membe alikabidhi fedha hizo kwa kutoa shilingi milioni 8 taslim na kuahidi kumalizia shilingi milioni 7 baada ya wiki moja.
Fedha hizo zilizotolewa ni kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi huo ambao unatarajia kumalizika mwezi Disemba mwaka huu na utagharimu shilingi milioni 35 hadi kukamilika kwake.
Waziri Membe, alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) kiko katika harakati za kukabiliana na uchaguzi Mkuu hivyo ni vyema wakati wa kupiga kura ya maoni ya kutafuta wagombea wanachama wahakikishe wanachagua viongozi wataoweza kuchagulika katika nafasi yoyote.
Alisema CCM katika uchaguzi mkuu ujao kimeamua kutanua demokrasia katika kupata wagombea, lakini ikiwa hawatazingatia kuitumia vyema kuchagua viongozi bora watakuwa wanafanya makosa.
Alisema jambo la msingi ambalo wanapaswa kulizingatia wakati wakifanya uteuzi wa viongozi wao ni kuhakikisha wanachagua viongozi ambao watakuwa wanateulika katika ngazi zote.
Alisema hatua hiyo ni muhimu kuzingatiwa na wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwani viongozi bora wataowachagua ndio wataompa nafasi nzuri ya kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu Rais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema Chama cha Mapinduzi kinafahamu umuhimu wa maendeleo na kuwepo kwa ukumbi huo wa mikutano utaweza kuchangia kuinua shughuli za chama.
Membe alisema wazo la viongozi wa Jimbo hilo kuamua kuanzisha ukumbi huo ni moja ya jambo zuri linalostahiki kupongezwa.
Mjumbe huyo katika sherehe hiyo pia aliwakabidhi kadi wanachama wapya 210 wa Jimbo hilo pamoja na kukubaliana kushirikiana kati ya Jimbo la Kitope na Jimbo lake cha Mtama liliopo Kusini mwa Tanzania.
Naye mfanyabiashara Mohammed Raza alichangia ujenzi wa jengo hilo kwa kutoa mabati 50 pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo kikombe, mipira na jezi kwa timu 21 za Jimbo hilo.
Aidha Raza alitoa mchango kama huo wa vifaa vya michezo kwa timu za Jimbo analoliongoza Waziri Membe la Mtama.
Baada ya kukabidhi msaada huo Raza aliwaeleza wanachama hao kuwa hatua yake ya kutoa msaada huo ni muhimu na kukuza ushirikiano kati ya wafanyabiashara na wananchi.
Alisema bila ya wananchi kuchangia kutumia huduma zao wafanyabiashara wasingeweza kunufaika na ndio maana ameamua kutoa misaada kwa wananchi kwa vile wanathamini mchango wao.
Hata hivyo Raza alionya wafanyabiashara waliojijengea tabia ya kuwakandamiza wananchi kwa kuwauzia bidhaa zao kwa bei ya juu kiasi cha kuwafanya maisha kuyaona magumu.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Idd, alimpongeza Waziri Membe kwa moyo wake aliouonesha wa kulichangia Jimbo hilo jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa pande mbili za Muungano.
Alisema mchango alioutoa ni mwanzo mwema wa kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo ambalo litawasaidia wananchi wa Jimbo hilo kwa vile hivi sasa wamekuwa wakifuata huduma za ukumbi wa mikutano maeneo ya mbali.
No comments:
Post a Comment